Michezo

Bingwa mtetezi Kamworor nje ya Nusu-Marathon Duniani

September 30th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi sasa kuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya wanaume, Geoffrey Kamworor hatatea taji la Riadha za Nusu-Marathon Duniani hapo Oktoba 17, 2020 mjini Gdynia, Poland.

Bingwa huyu wa Riadha za Nusu-Marathon Duniani mwaka 2014 (Copenhagen, Denmark), 2016 (Cardiff, Wales) na 2018 (Valencia, Uhispania) alikuwa amedokeza majuzi kuwa hana uhakika kama atakuwa fiti kushindana mjini Gdynia baada ya kuumia kichwa na kifundo alipogongwa na pikipiki kutoka nyuma akifanya mazoezi kwenye barabara ya Kaptagat-Eldoret mnamo Juni 25.

Tovuti ya Race Results Weekly (RRW) imethibitisha Jumatano kuwa mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 27 hatakuwepo kwenye orodha ya washiriki kwa sababu hajapona kabisa.

“Ni aibu kubwa kuwa Geoffrey Kamworor hawezi kutetea taji la dunia la Nusu-Marathon mjini Gdynia. Ushindi wake mjini Valencia miaka miwili iliyopita ulikuwa wa kihistoria,” tovuti hiyo ilisema.

Mnamo Juni, bingwa wa mbio za kilomita 42 za New York Marathon mwaka 2017 na 2019 Kamworor alitibiwa katika hospitali ya St Luke’s mjini Eldoret katika kaunti ya Uasin Gishu baada ya ajali mbaya ya pikipiki. Aliruhusiwa kuendelea na matibabu nyumbani.

Katika ajali hiyo, mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya dakika 58:01 aliyoweka jijini Copenhagen mwaka 2019, alijeruhiwa kichwa na kifundo. Mwendeshaji huyo wa pikipiki hiyo aliisimamisha na kumkimbiza hospitali alikolazwa na kufanyiwa upasuaji.

Kamworor alitarajiwa kutoana kijasho na Mganda Joshua Cheptegei anayepigiwa upatu kuponyoka na taji mjini Gdynia.

Mbali na Uganda, ambayo pia itawakilishwa na Abel Chebet, Moses Kibet, Jacob Kiplimo na Stephen Kissa, mataifa mengine ambayo yametaja watimkaji wao kushiriki makala hayo ya 24 ni Canada, Uingereza, Poland na Uhispania.  Kenya iko katika orodha ya mataifa ambayo bado hayajatangaza vikiosi vyao vitakavyoshiriki mbio hizo za kifahari.