Kimataifa

Binti aliyekumbatia mwanamuziki ashtakiwa kumdhulumu kimapenzi

July 19th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

TA’IF, SAUDI ARABIA

MSHICHANA anakabiliwa na mashtaka ya dhuluma za kimapenzi baada ya kumkumbatia mwanamuziki wa kiume.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha mwanamuziki mashuhuri wa Kiarabu, Majid al-Mohandis, akiimba kwenye tamasha.

Ghafla msichana aliyevaa buibui alitoka kwenye umati akakimbia katika jukwaa ambapo mwanamuziki huyo alikuwepo na kumkumbatia.

Ilibidi maafisa wa usalama waingilie kati kumwondoa jukwaani kwa lazima kwani alikuwa amemkwamilia mwanamuziki huyo.

Mashirika ya habari yalisema polisi walimkamata kwa sababu alikiuka sheria za nchi hiyo zinazokabiliana na dhuluma za kimapenzi.

Ilisemekana kuwa endapo atapatikana na hatia, msichana huyo ambaye haijafahamika ni wa umri gani anaweza kuhukumiwa miaka miwili gerezani na kutozwa faini ya Pauni 20,000 (Sh2.66 milioni).

-Imekusanywa na Valentine Obara