Michezo

Binti mkali wa michezo ya kiume chuoni

December 11th, 2019 3 min read

NA STEVE MOKAYA

ELIZABETH Wairimu ni binti mwenye mataji kadhaa. Mbali na kuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika kozi ya uanahabari chuoni TUM, binti huyu ni mwanaspoti mkereketwa wa aina mbili za michezo.

Anashiriki mchezo wa uendeshaji baiskeli pamoja na ule wa kuteleza barabarani kwa kutumia viatu spesheli vyenye magurudumu maalum, almaarufu “roller skating”.

Na kwake si kushiriki tu. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ameshinda mataji kadhaa, pamoja na kutuzwa vyeti kadhaa.

Binti huyu mwenye umri wa miaka 21 alianza kuvutiwa na mchezo wa kuendesha baiskeli akiwa mtoto. Ila baada ya kumaliza kidato cha nne, marafiki wenza na jamaa sawia walimshawishi apeleke talanta yake katika hatua nyingine, na hapo ndipo mkoko ukaalika maua.

“Baada ya KCSE, wazazi wangu waliniambia kuwa niko na talanta na inahitaji kukuzwa zaidi, badala ya kutoichukulia maanani kama nilivyokuwa nikiichukulia,” Liz anaeleza.

Nyumbani kwao Naivasha, kulikuwa na marafiki waliokuwa wanashiriki mchezo huu wa kuendesha baiskeli na wakamwelekeza hadi akajisajili rasmi katika shirikisho la waendeshaji baiskeli nchini. Hivi sasa, yeye ni mmoja wa wanachama wa klabu ya Kenya Riders.

Klabu hii hufanyia mazoezi yake mengi katika kambi ya Itein. Hata hivyo mara nyingi yeye huwa hayupo huko kwa sababu ya masomo.

Hata hivyo, kocha wake anafuatilia kwa makini sana mchezo wake, japo yuko mbali na wengine. Kufikia sasa, ameshiriki mashindano kadhaa ya kitaifa na kuibuka kidedea katika mawili yao.

“Katika mwaka wa 2017 na 2018, nilishiriki katika mbio za ‘Touring Machakos’ na kuibuka nambari moja katika kitengo cha wasichana. Kadhalika, nilishiriki mashindano ya “Farmers’ Choice” na kuwa nambari tatu,” anaeleza.

Liz akiwa mazoezini. Picha/ Hisani

Wasemao husema kuwa hakuna kizuri kijacho rahisi. Kwa binti Liz, msemo huu ni kweli, kwani amezipitia changamoto si haba. Anadokeza kuwa inambidi aasi usingizi wake mapema sana kama saa kumi ushei asubuhi ili akaende kufanya mazoezi.

Fauka ya hayo, hatumii wikendi zake kulala ama kuzuru ufuoni kama wengi wa wanafunzi chuoni mwao. Badala yake, yeye hutumia wakati huo katika kufanya mazoezi katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Kenya, ikiwemo Kaloleni, Kilifi, na Kwale.

Kutokana na haya, anafafanua kuwa amewapoteza marafiki wake wengi, kwa sababu baadhi yao hushindwa kuelewa kuwa inabidi afanye mazoezi.

“Wengine wao hudhani kuwa nawakwepa lakini sasa nifanye nini? Lazima tu nifanye mazoezi kwa sababu nataka kukua na pia kukuza mchezo wangu,” anasema.

Isitoshe, inambidi atafute vijana wa kiume wenzake ili wakashiriki naye mazoezi, kwa sababu si wasichana wengi wafanyao mchezo huu wa kuendesha baiskeli. Wakati mwingine, anapata changamoto pale baiskeli yake inapopatwa na shida na yu mazoezini.

Wazazi wake wamekuwa nguzo muhimu sana kulingana na yeye.

“Wao ndio walinunulia baiskeli zangu za mashindano. Wakati ninapohitajika kuenda kushiriki mashindano, pia wananitumia hela za matumizi na malazi. Wako na mimi kabisa, ilimradi mchezo huu hauathiri masomo yangu kwa vyovyote vile,” anasema.

Mbali na kuwa staa katika mchezo wa kuendesha baiskeli, Liz Wairimu anang’aaa katika mchezo wa kuteleza barabarani.

Alijitosa katika mchezo huu katika mwaka wa elfu mbili na kumi na nne. Kama mchezo wa kuendesha baiskeli, amejisajili katika shirikisho la mchezo huu, na anashiriki mashindano na mazoezi. Hivi sasa yeye ni mwanaklabu ya ‘Sprint Skating Club kenya’.

Umuhimu wa mchezo huu wa kuteleza ni kuwa klabu yake huwasaidia wachezaji vifaa vya mazoezi na viatu vya mashindano.

Liz aliposhinda tuzo. Picha/ Hisani

Huku pia ameshiriki mashindano mbalimbali ila amekuwa akiibuka nambari tatu tu. “Sijui mbona sipiti namabri ya tatu, lakini nazidi kujikaza tu,” anaongeza akicheka.

Hata hivyo, mchezo huu una hatari ya kupatwa na ajali na kuumia sana, hasa iwapo mshiriki hana vyombo husika. Hapa anasimulia ajali iliyowahi kumpata.

“Tulikuwa tumeenda katika mashindano jijini Kisumu. Wakati huo sikuwa nimevalia nguo zangu na vyombo vya kunikinga dhidi ya kupatwa na majeraha iwapo ajali ingetokea. Kwa bahati mbaya nilianguka na kuumia vibaya sana. Tangu siku hiyo huwa niko makini sana kuvalia nguo zinazonikinga, pamoja na kofia,” anasema.

Chuoni TUM anakosomea, amejiunga na wanafunzi wengine washirikiao mchezo huo na pamoja wanafanya mazoezi. Hata hivyo, yeye anapendelea kuendesha baiskeli kuliko kuteleza barabarani.

Hivi sasa Liz anatazamia kuhamia katika taifa la Ujerumani ama Uholanzi ili akaikuze talanta yake hata zaidi, na azamie mchezo wa uendeshaji baiskeli kabisa.

Hata kama anasomea kozi ya uanahabari, bado angali kuamua sehemu ya taaluma hiyo ambayo angependa kujihusisha nayo. Japo anasema kuwa kuwa ni mahiri katika kupiga picha. Kadhalika, ananuia kusomea uzamifu katika uanahabari kabla aanze ajitose ulingoni.

Pia mbali na mataji na vyeti alivyovishinda kutokana na michezo yake, amezuru miji mbalimbali humu nchini, ili kushiriki michezo hii.

Baadhi yao ni Malindi, Nakuru, Murang’a, Nairobi, Kisumu, Mombasa, miongoni mwa mingine. Pia anatazamia kufanya safari ya barabarani kwa baiskeli kutoka jijini Mombasa hadi Dar es Salaam, Tanzania.

“Siamini kuwa maisha ni masomo tu. Na hata kama uko shuleni unasoma, ni vizuri kama uko na talanta uikuze. Talanta pia husaidia. Lakini ilimradi talanta yako isilemee masomo yako,” anamalizia.