Habari Mseto

Binti mwenye 'nguvu za kishetani' afukuzwa shuleni

July 9th, 2018 2 min read

Na VIVERE NANDIEMO

MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 katika eneo la Suna Magharibi, Kaunti ya Migori, anataabika baada ya kufukuzwa shuleni kufuatia madai kuwa anaabudu shetani.

Mwanafunzi huyo wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Nyamome alidaiwa kuwa mwanachama wa kikundi cha kuabudu shetani na alihusika kusajili wanafunzi wenzake kujiunga na kikundi hicho.

Ilisemekana shule iliamua kumfukuza kwa vile alikuwa akizimia mara kwa mara kutokana na tatizo lisilojulikana.

“Alikuwa akianguka kisha anaanza kutamka mambo ambayo hayaeleweki kama kwamba anawasiliana na mapepo. Amekuwa akifanya hivi kwa muda mrefu sasa na kushtua wanafunzi wenzake. Pengine hii ndio maana wasimamizi wa shule waliamua kumfukuza,” mmoja wa walimu wa shule hiyo aliyeomba asitajwe jina, akasema.

Msichana huyo alifukuzwa shuleni wiki tatu zilizopita na amekuwa nyumbani kwa muda huo wote.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, alikanusha madai kwamba ni mwanachama wa kundi la kuabudu shetani.

“Ninalaumiwa kwa jambo ambalo hata silielewi. Ninapenda kwenda shuleni lakini sasa nimezuiliwa. Huwa nakaa tu nyumbani bila chochote cha kufanya,” akasema kwa kilio.

Mamake pia alimtetea na kusema shule hiyo ingewasiliana naye kwanza kabla kuchukua hatua ya kumkatizia masomo.

“Ninaomba usaidizi. Sidhani kama binti yangu huabudu shetani. Ninaomba shule hiyo imruhusu aendelee na masomo yake ninapotafuta msaada ya kimatibabu kwa hali yake,” akasema.

Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa shule hiyo, Bw Alex Siro, alisema wasimamizi walimfukuza baada ya kuthibitisha alikuwa na “nguvu za kishetani”.

“Alipatikana akifanya mambo yasiyo ya kawaida huku akijaribu kusajili wanafunzi wengine kwa mienendo yake. Tulichukua hatua hii ili kuondolea watoto wengine hofu kwani wengi wao walikuwa hawaji shuleni kwa sababu wanamwogopa msichana huyo,” akasema.

Kwenye barua ya kumfukuza shuleni iliyoandikwa Julai 2, 2018, Bw Siro alisema uamuzi ulifanywa na bodi ya usimamizi wa shule na kumshauri mamake ampeleke akafanyiwe maombi.

Mamake alitoa wito kwa Wizara ya Elimu iingilie kati ili binti yake aruhusiwe kurudi shuleni.

, huku watetezi wa haki za watoto wakikashifu wasimamizi wa shule kwa hatua waliyochukua kwani huenda tatizo lake ni la kiafya.