Habari Mseto

Bintiye bwanyenye wa Pelikan Signs ashtakiwa kughushi wosia kwa nia ya kuibia dada zake

May 6th, 2024 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

BINTIYE mmiliki wa kampuni ya Pelikan Signs Limited Jumatatu alishtakiwa kughushi Wosia wa baba yao ili kuwatapeli dada zake wawili mali.

Dinta Devani Pathiana pamoja na mumewe  Abhay Singh Pathiana walishtakiwa pamoja na Samuel Ndingure na Addah Nduta Ndambuki.

Wanne hao walikana shtaka la pamoja la kughushi Wosia wa marehemu Balkrishna Ramji Haribhai Devani kudanganya walikuwa wameteuliwa kuwa Wakurugenzi wa Pelikan.

Hakimu mkuu Bernard Ochoi alielezwa wanne hao hawakuwa wameteuliwa kuwa wasimamizi wa mali ya Devani aliyeaga Juni 7, 2019.

Hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka kwamba wanne hao walighushi na kubadilisha Wosia huo Juni 5, 2019.

Dinta alishtakiwa alighushi na kubadilisha Wosia huo baba yake alipokuwa mgonjwa mahututi akiwa amelazwa chumba cha kuhifadhi wagonjwa mahututi.

Washtakiwa walikana kujiandikia hisa za kampuni ya Pelikan Signs kinyume cha sheria katika afisi ya Msajili wa Kampuni.

Dinta alishtakiwa kujipatia kampuni ya Silverstar Properties Limited bila idhini ya baba yake.

Wakili Danstan Omari anayewakilisha Dinta na  Abhay aliomba waachiliwe kwa dhamana akisema “akaunti zao zilifungwa na Mahakama kuu baada ya habari kutolewa walikuwa wameghushi Wosia wa bwanyenye huyo.”

Bw Ochoi aliwaachilia Dinta, Abhay na Nduta kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu ilhali Ndinguri aliyeshtakiwa wiki iliyopita alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh1 milioni.