Bintiye Keroche alikiri Lali alimpagawisha kwa mapenzi, nduguye aambia mahakama

Bintiye Keroche alikiri Lali alimpagawisha kwa mapenzi, nduguye aambia mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

MMOJA wa wakurugenzi wa kampuni ya Keroche Breweries aliyekufa, Tecra Muigai alikuwa amekiri kwa nduguye kuwa alikuwa amepagawa na mapenzi ya Omar Lali Omar, na kila alipojaribu kumuacha alishindwa.

Akitoa ushahidi kwenye uchunguzi wa mahakama kuhusu kifo cha Tecra, nduguye marehemu, James Karanja alieleza mahakama kwamba alikuwa ametumwa na wazazi wake Lamu kumwashawishi dada yake avunje uhusiano na Lali, lakini ikashindikana.

“Tecra alinifichulia kwamba alikuwa amepagawa na mapenzi ya Lali na kila alipotaka kumwacha alikuwa anashindwa,” akasema Bw Karanja.

“Rakifiye Tecra kwa jina Yvonne alinieleza kuwa Lali alikuwa na uhusiano na wanawake wazungu na waafrika, na akanigusia kuwa ilihofiwa alikuwa anatumia ushirikina kuwavutia wanawake,” akaongeza Bw Karanja.

Alisema familia yao ilikuwa ikitaka Tecra awachance na Lali kwa sababu alikuwa na umri mkubwa kumliko Tecra. Tecra alikuwa na umri wa miaka 30 naye Lali alikuwa na 50.

Wakati huo huo, mahakama iliagiza Lali afike kortini kuhojiwa kuhusiana na kifo hicho.

Hakimu Zainab Abdul alisema Lali ametajwa na mashahidi 11 kuhusiana na kifo cha mpenziwe.

Wengine ambao wameitwa na mahakama ni Kusai Lali Omar, Ali Bakari Mohamed, Abdul Akini Lali Omar, Yahya Salim Mohamed, Ahmed Ali Salim na Mohamed Salim Muhanji.

Wakili wa familia ya marehemu Tecra, Bw Elisha Ongoya, alieleza mahakama kwamba kulingana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Lali atahitajika kujitetea.

Wakili huyo alisema afisi ya DCI ilipeleka gari la kuwasafirisha mashahidi kutoka Lamu lakini wakakataa kuabiri ili kufika kortini kutoa ushahidi.

“Afisi za Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na DCI zilikuwa zimetayarisha makazi ya mashahidi hawa wakiwa Nairobi. Walikataa kuabiri gari iliyopelekwa kuwachukua. Sasa naomba mahakama itoe agizo wafike kortini kutoa ushahidi,” alisema Bw Ongoya.

Afisi ya DCI Lamu imeagizwa isaidie afisa anayechunguza kesi hiyo kuhakikisha mashahidi hao wamefika kortini Mei 4, 2021, uchunguzi utakapoendelea.

You can share this post!

Rais azima mikutano mikubwa ya kisiasa kwa siku 30

ODM yadai viongozi 4 wamedandia handisheki kujifaidi