Habari za Kitaifa

Bintiye Rais Moi, June Chebet aaga dunia

April 11th, 2024 1 min read

NA FRANCIS MUREITHI

BINTIYE rais mstaafu hayati Daniel Moi, Bi June Chebet aliaga dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 60.

Bi Chebet alikuwa binti wa kupanga wa Rais Moi japo ni wachache waliofahamu hivyo, kulingana na duru za karibu.

Mhudumu aliyewahi kufanya kazi katika boma la Rais Moi, Kabarak, Kaunti ya Nakuru, alisema Bw Moi alimchukua Bi Chebet katika miaka ya 60 akiwa na umri wa miaka minne.

Wakati huo, Bw Moi aliyekuwa amejaaliwa binti zake Jenifer na Doris, alikuwa anahudumu kama Naibu Rais kuanzia 1967 hadi 1978 chini ya Rais Jomo Kenyatta.

“Sijui Mzee Moi alimchukua June kwa hali ipi. Lakini ninachojua kwa hakika Mzee Moi hangempanga June bila idhini ya mke wake marehemu Lena,” zilisema duru.

“Mzee Moi hakuwahi kutangaza kuhusu kumpanga June na hakuwa na sababu yoyote ya kufanya hivyo kwa sababu hakuwa anaomba msamaha kwa yeyote na June tayari alikuwa sehemu ya familia.”

Marehemu June aliwahi kuolewa na Rubani kwa jina John Okubasu, mwanawe jaji mstaafu mashuhuri, Emmanuel Okubasu, waliyejaaliwa pamoja binti.