Habari Mseto

Biwi la simanzi mbunge wa Kabuchai akifa

December 5th, 2020 1 min read

Na BRIAN OJAMAA

MBUNGE wa Kabuchai, James Mukwe Lusweti (pichani) alifariki Ijumaa adhuhuri katika Nairobi Hospital baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kifo chake kimetokea wakati ambapo Mbunge wa Matungu, James Murunga anazikwa leo Jumamosi.

Mbunge huyo anayehudumu kwa muhula wa pili aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Ford-Kenya, amekuwa akiugua yabisi kavu na jongo (arthritis) kwa miaka mingi.

Duru za karibu na mbunge huyo zilieleza Taifa Leo kwamba mbunge huyo alisafirishwa kwa ndege mnamo Alhamisi ili kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa kimatibabu lakini akapata matatizo ya kupumua.

Alikimbizwa katika Nairobi Hospital na akalazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), ambapo aliaga dunia. Bw Lusweti alipata wadhifa wa ubunge mnamo 2013 baada ya kuhudumu mihula mitatu kama diwani.

Katika ujumbe wake wa kutuma rambirambi, Rais Uhuru Kenyatta alimsifu Bw Lusweti kama mwanasiasa mpole lakini mwenye ushawishi mkubwa mashinani ambaye miradi yake ya kijamii ilisaidia kuboresha maisha ya familia nyingi Kabuchai na Kaunti ya Bungoma kwa jumla kutoka kwa ufukara.