Habari Mseto

Biwi la simanzi mwanafunzi, 12 aliyejitoa roho akizikwa Nakuru

November 28th, 2020 1 min read

Na JOHN NJOROGE

HUZUNI Ijumaa ilitanda katika mtaa wa Kasarani, mjini Elburgon, katika Kaunti ya Nakuru wakati wa mazishi ya mwanafunzi wa darasa la tano aliyejitia kitanzi juma moja lililopita.

Familia, jamaa na marafiki walitirikwa na machozi wakati wa mazishi hayo ya Raban Kimungu Muiruri, 12. Mwili wa marehemu ulipatikana umening’inia kwenye paa la nyumba Jumapili iliyopita usiku.

Babake Paul Muiruri Wang’ombe, 57 alimrejelea kama mtoto mngwana, mtiifu na mwenye bidii ambaye alipenda masomo na kutumia muda wake mwingi na wanafamilia wake.

Marehemu alikuwa kitinda mimba kwenye familia hiyo iliyojaaliwa watoto 10.

“Nimefiwa na mtoto ambaye sikuwahi kugombana naye tangu utotoni. Kabla ya mauti yake, alikuwa amefurahi na hata alimtaka mamake ampikie chapati,” akasema Bw Wang’ombe. Baba huyo aliwataka wazazi wafuatilie mienendo ya wanao kwa kuwa bado ni wadogo na wanahitaji mwongozo mzuri.

Rafikiye marehemu Maxwell Mwangi ambaye pia walikuwa naye darasa moja alibubujikwa na machozi huku akisema kifo hicho kimemwaathiri sana kwa kuwa hakukitarajia.

“Aliniambia tutakutana baadaye kwa kuwa alikuwa anaenda mahali ambapo hakufichua. Nilitatizika sana hadi nikasikia mauti yake siku iliyofuatia,” akasema.