Michezo

Blaise Matuidi asajiliwa rasmi na Inter Miami ya Amerika

August 13th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Blaise Matuidi ameingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Inter Miami kinachoshiriki kipute cha Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Matuidi aliagana na Juventus mnamo Agosti 12, 2020, baada ya kuafikiana kutamatisha mkataba wake wa mwaka mmoja uliokuwa umesalia.

Matuidi, 33, alikuwa sehemu ya timu ya taifa iliyonyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

Nyota huyo aliwahi kucheza na David Beckham ambaye ni miongoni mwa wamiliki wa Inter Miami kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Juventus mnamo 2017.

“Natarajia kunyanyua mataji ya haiba kubwa nikivalia jezi za Inter Miami. Ni fursa nzuri ya kukabiliana na changamoto mpya,” akasema Matuidi.

Inter Miami ambao huu ni msimu wao wa kwanza kwenye kivumbi cha MLS kitakachorejelewa mnamo Agosti 22, 2020, walipoteza mechi zote tano za awali kabla ya soka ya ligi hiyo kusitishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona.

“Ni tija na fahari kubwa kujivunia huduma za Matuidi – rafiki yangu niliyewahi kucheza naye kambini mwa PSG,” akasema Beckham ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza.

“Ni mwanasoka anayejivunia utajiri mkubwa wa kipaji. Kuwa na mshindi wa Kombe la Dunia kambini mwetu ni kitu kizuri cha kujivunia kwetu sisi wamiliki wa kikosi na mashabiki wetu,” akaongeza Matuidi.

Matuidi ambaye kwa sasa atavalia jezi nambari nane mgongoni kambini mwa Inter Miami, amekuwa mshindi wa mataji ya Ligi Kuu kwa misimu saba kati ya minane iliyopita.

Anajivunia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mara nne akivalia jezi za PSG na Ligi Kuu ya Italia (Serie A) akiwa mchezaji wa Juventus.

Alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Ufaransa kilichowapepeta Croatia 4-2 katika fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018.

Nyota huyo alisajiliwa na Juventus kutoka PSG mnamo 2017 kwa kima cha Sh3.9 bilioni na Inter Miami kwa sasa wamejinasia huduma zake kwa Sh3.4 bilioni.

Fedha hizo zinamfanya kuwa miongoni mwa wanasoka ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi hicho cha Amerika.