Michezo

Blak Blad yailipua Western Bulls 44-0 katika Kenya Cup

January 19th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Blak Blad walifufua matumaini ya kukwepa kuangukiwa na shoka baada ya kulipua Western Bulls 44-0 kwenye Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta jijini Nairobi.

Mchezaji Arcadius Khwesa alikuwa shujaa wa Blak Blad akichangia miguso mitatu muhimu.

Ushindi huu unatarajiwa kuondoa Blak Blad katika mduara hatari wa kutemwa na kwa wakati huo na kusukuma Bulls kutoka kaunti ya Kakamega katika maeneo hayo.

Bulls, ambayo imerejea katika Ligi Kuu msimu huu baada ya kushushwa msimu 2016-2017, iliingia mchuano huo wa raundi ya 11 ikifunga mduara wa 10-bora kwa alama 13 katika ligi hii ya klabu 12 nayo Blak Blad ilishikilia nafasi ya 11 kwa alama nane.

Uwanjani Nairobi Railway, wenyeji Mwamba walikubali kichapo cha alama 18-13 kutoka kwa Nakuru iliyostahimilia mashambulizi makali katika dakika za lala-salama.

Baadhi ya wafungaji wa alama za Nakuru, ambayo iliongoza 18-3 wakati wa mapumziko, walikuwa Collins Onyango, Oscar Ouma na Emmanuel Mboya.

Nayo Impala Saracens ilitolewa kijasho chembamba na wageni wake Menengai Oilers kabla ya kuwashinda 37-29 uwanjani Impala Club. Timu hizi zilibadilishana uongozi mara kadha na wakati mmoja zilikuwa 10-10 kabla ya Impala kuchukua kufungua mwanya kabisa baada ya kujitosa mbele 20-15.

Uwanjani Jamhuri Park jijini Nairobi, wenyeji Nondies waliaibishwa mbele ya mashabiki wao kwa alama 37-11 dhidi ya majirani Homeboyz.

Mjini Kisumu, wenyeji Kisumuu waliona cha mtema kuni dhidi ya mabingwa watetezi KCB baada ya kukanyagwa 55-7.

Tukienda mitamboni, wenyeji Kabras Sugar walikuwa wanaongoza Kenya Harlequin kutoka Nairobi kwa alama 27-3 uwanjani Kakamega Showground.