Michezo

Blatter ataka Kombe la Dunia 2026 liandaliwe Morocco

February 26th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

‘FISADI’ Sepp Blatter anapigia debe Morocco kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2026.

Rais huyu wa zamani wa Shirikisho la Soka duniani (FIFA) haungi mkono ombi la Marekani, Mexico na Canada kutuma ombi la kuandaa fainali hizo kwa pamoja.

Anaona Bara Afrika na hasa Morocco inafaa kupewa nafasi hiyo.

Raia huyu kutoka Uswizi alipigwa marufuku ya miaka sita na FIFA kwa ufisadi mwaka 2015 baada ya Marekani kuongoza uchunguzi uliomfanya ang’atuke mamlakani.

Aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter hapo Februari 22, 2018 kwamba FIFA ilikataa maandalizi ya pamoja ya kombe hili hadi mwaka 2018 na kwamba Morocco ni chaguo bora.

Baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2002 nchini Japan na Korea Kusini, FIFA ilirejelea mfumo wa taifa moja kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia. Hata hivyo, makala ya mwaka 2026 yatakuwa tofauti kwa sababu washiriki watyaongezeka kutoka mataifa 32 hadi 48.

Morocco iliomba maandalizi ya Kombe la Dunia mwaka 1994, 1998, 2006 na 2010, lakini bila mafanikio. Ilishindwa na Marekani kura 10-7 katika ombi lake la mwaka 1994.

Brazil ilipata kura mbili mwaka huo. Mwaka 1998, Morocco ilipoteza kwa kura 12-7 dhidi ya Ufaransa baada ya Uswizi, Uingereza na Ujerumani kujiondoa. Ujerumani ilipata haki za kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2006 kwa kuzoa kura 10, huku Afrika Kusini, Uingereza na Morocco zikiambulia kura sita, tano na mbili, mtawalia.

Morocco ilijaribu bahati yake tena mwaka 2010, lakini ombi lake likashindwa na lile la Afrika Kusini kwa kura 14-10. Misri ilipata kura sifuri. Tunisia na Libya, ambazo zilituma ombi moja, zilijiondoa sawa na Nigeria.