Boateng kukosa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Bayern Munich na Tigres baada ya mchumba aliyemtema wiki iliyopita kuaga dunia

Boateng kukosa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Bayern Munich na Tigres baada ya mchumba aliyemtema wiki iliyopita kuaga dunia

Na MASHIRIKA

BEKI Jerome Boateng hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Hansi Flick wa Bayern Munich kwenye fainali ya Kombe la Dunia kwa Klabu itakayowakutanisha leo usiku na Tigres UANL ya Mexico.

Hii ni baada ya difenda huyo raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 32 kuondoka nchini Qatar na kurejea nyumbani kutokana na kifo cha aliyekuwa mpenzi wake Kasia Lenhardt aliyetememana naye wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa Flick, Boateng ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester City, aliomba idhini ya kuondoka kambini ili kurejea Berlin baada ya mwili wa kipusa huyo kupatikana kwenye mojawapo ya makasri yanayomilikiwa na mwanasoka huyo nchini Ujerumani.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Boateng alifichua kwamba alikuwa ametengana rasmi na Kasia, 25, baada ya kuhusiana kimapenzi na mwanamitindo huyo kwa kipindi cha miezi 15.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Kasia aliaga dunia mnamo Jumanne , siku ambapo mwanawe Noah aliyepatikana katika uhusiano wa awali aliokuwa nao na mwanamume mwingine aliyedumu naye kwa miaka mitatu, alikuwa akiadhimisha miaka sita ya kuzaliwa.

Gazeti la Bild nchini Ujerumani liliripoti mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Kasia alihusika kwenye ajali ya barabarani akiendesha gari la Boateng mnamo Januari 5. Gari hilo liliharibika kiasi cha kutokarabatika tena.

Kwa mujibu wa The Sun, Kasia ambaye ni raia wa Poland, alikuwa amechanja chale za kudumu zenye maandishi ya jina la Boateng kwenye kifua chake, na kiini cha kutemana kwake na sogora huyo ni jicho la nje la Boateng.

Kasia ambaye pia ni mwanahabari, aliwahi kushiriki mashindano ya uanamitindo nchini Ujerumani mnamo 2012 na akaambulia nafasi ya nne. Boateng ana watoto pacha wa kike waliozaliwa mnamo 2011 na mvulana aliyezaliwa mnamo 2015. Watoto hao walizaliwa na wanawake wawili tofauti.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Azidi kumiminiwa sifa kwa kutumia talanta yake katika...

Ongwae asalia nje Bungei aking’ara katika ushindi wa...