Kimataifa

Bobi Wine aambia Rais ang’atuke

March 26th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MBUNGE wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama ‘Bobi Wine’ amesema kwamba uongozi wa Rais Yoweri Museveni unaelekea kuisha.

Mbunge huyo alisema wakati wa kiongozi huyo mkongwe kung’atuka uongozini umefika huku taifa hilo likijitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa urais 2021.

“Nakwambia wewe Museveni, siku zako uongozini ni chache. Ni vipi unasema kwamba ulienda vitani kupigania demokrasia ambayo hata hauzingatii katika chama chako cha NRM?” akauliza mbunge huyo.

Alitoa kauli hiyo katika eneo la Arua, ikiwa mara yake ya kwanza kurejea humo tangu alipokamatwa mnamo Agosti 13 mwaka uliopita.

Alikuwa amehudhuria makaribisho ya mbunge wa eneo hilo, Kassiano Wardi, waliyekamatwa pamoja naye.

Wiki iliyopita, wabunge wa chama cha NRM walimpitisha Rais Museveni kama mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.

Ikiwa ataibuka mshindi, basi atakuwa miongoni mwa viongozi ambao wamehudumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Kwenye hotuba aliyotoa baada ya kupitishwa, Rais Museveni, ambaye ana miaka 74, alisema yuko tayari kuliongoza taifa hilo kwa kipindi kingine.

“Niko tayari kuendelea kuwatumikia Waganda kama kiongozi wao, ikiwa watanipa jukumu hilo itakapofika 2021. Ningali na uwezo wa kuwaongoza,” akasema Rais Museveni, huku akishangiliwa na wabunge wa chama hicho.

Wine tayari ametangaza nia ya kuwania urais.

Robert Kyagulanyi maarufu kama ‘Bobi Wine’. Picha/ Maktaba

Kwenye hotuba yake, mbunge huyo aliwaomba raia kujisajili kwa wingi na kuchukua vitambulusho ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

“Ninawaomba muonyeshe ushujaa kama mliodhihirisha mliponichagua kama mbunge huru. Zingatieni haki zenu. Mnapaswa kujitolea na kusimama nasi kama mlivyofanya Agosti tulipokamatwa,” akasema.

Amkosoa Rais

Alimkosoa vikali Rais Museveni, ambaye awali alikuwa amemwambia kuangazia masuala ya muziki badala ya kujihusisha na siasa.

“Wakati wewe Museveni ulikuwa katika umri kama huu wangu, si ulijihusisha na kuchunga ng’ombe pekee? Sitazingatia wito wako, bali nitaendelea kuwatetea raia,” akasema.

Kiongozi mwingine wa upinzani, Jenerali Mugisha Muntu, aliseja kwamba wakati umefika ambapo raia wa Uganda wanapaswa kuwachagua viongozi wapya.

Aliwashauri kutumia uwezo wao kuwachagua viongozi ambao watashughulikia maslahi yao, wala si mamlaka wanayopata kuvuruga na kuwanyima haki zao.

“Mamlaka hayapo katika umiliki wa bunduki, mbali kwa wananchi. Utawala wa Museveni unaogopa kwani unafahamu kwamba umewakasirisha raia wengi kwa kuwanyima haki zao za kisiasa,” akasema.

Rais Museveni amekuwa akikosolewa kwa kuwahangaisha wapinzani wake, akitumia polisi na vikosi vingine vya usalama kuwakabili kila mara wanapoandaa maandamano ama mikutano ya kisiasa.