Kimataifa

Bobi Wine aeleza anavyomheshimu Museveni

October 3rd, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

MBUNGE wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi almaarufu kama Bobi Wine, amesema hawezi kumkosea heshima Rais Robert Museveni, hata anapopitia masaibu mengi mikononi mwa serikali kwa kutetea haki za kidemokrasia.

Mbunge huyo ambaye alikamatwa na kupigwa na maafisa wa polisi miezi miwili iliyopita alieleza kwamba juhudi zake za kutetea haki Uganda hazimlengi Museveni kibinafsi bali mageuzi yatakayoleta afueni kwa raia wote wa Uganda.

‘Ninapokutana naye huwa namsalimia kwa mkono kwa heshima kama rais. Singependa hatua zangu zitazamwe kama makabiliano kati yangu na Museveni. Hili ni suala kubwa kultuliko sisi kibinafsi,’ akasema mwanamuziki huyo wa zamani ambaye Museveni awali alikuwa amemtaja kuwa ‘mjukuu mtundu’.

Kwenye mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la NTV, alikashifu serikali kwa kukosa kutoa ripoti rasmi kuhusu matukio yaliyoshuhudiwa Agosti wakati wa uchaguzi wa ubunge katika eneo la Arua Municipality ambapo dereva wake, Yasin Kawuma, aliuawa kwa risasi.

Kyagulanyi alisema uamuzi wake wa kuachana na muziki kujiunga na siasa ulitokana na jinsi alivyoona hapakuwa na mtu yeyote wa kutetea haki za raia.

-Imekusanywa na Valentine Obara