Bobi Wine akerwa na kimya cha viongozi wa bara Afrika

Bobi Wine akerwa na kimya cha viongozi wa bara Afrika

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

ALIYEKUWA mwaniaji wa urais Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu Bobi Wine, ameshutumu vikali Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU) kwa kusalia kimya kuhusu masaibu yanayomkumba.

Bobi Wine ambaye amezuiliwa kuondoka nyumbani kwake tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu, wiki mbili zilizopita, jana alipata afueni baada ya Mahakama Kuu kuagiza maafisa wa usalama kumwachilia huru.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisema kuwa kuzuilia Bobi Wine nyumbani kwake katika eneo la Magere ni kinyume cha sheria.

Tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Januari 14, mwaka huu, ambapo Rais Yoweri Museveni aliibuka mshindi baada ya kupata zaidi ya asilimia 58 ya kura zilizopigwa, maafisa wa usalama wamekuwa wakizunguka nyumbani kwa Bobi Wine. Kiongozi huyo wa upinzani hakuruhusiwa kutoka au watu kuingia nyumbani kwake.

Balozi wa Amerika nchini Uganda ni miongoni mwa wageni waliozuiliwa kwenda kumtembelea Bobi Wine.

Mahakama Kuu ya Kampala ilitoa agizo hilo baada ya mawakili wa kiongozi huyo wa chama cha National Unit Platform (NUP) kuwasilisha malalamishi kortini wakitaka maafisa wa usalama wanaozunguka nyumbani kwa Bobi Wine waagizwe kuondoka.

Mawakili wa serikali walisisitiza kuwa Bobi Wine ataongoza maandamano iwapo ataruhusiwa kuondoka nyumbani kwake.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi, Bobi Wine alipata asilimia 35 ya kura zilizopigwa. Lakini chama cha NUP kimeshikilia kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya udanganyifu na wizi wa kura.

Jumatatu, Bobi Wine alimshutumu kiongozi wa Afrika Kusini ambaye pia ni mwenyekiti wa AU, Cyril Ramaphosa kwa kusalia kimya kuhusu unyanyasaji wa viongozi wa upinzani unaoendelea nchini Uganda.

Katika mahoajiano na shirika moja la habari la Afrika Kusini, Wine alisema kuwa Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU), Amerika na mashirika ya kijamii yamekemea dhuluma nchini Uganda lakini AU imesalia kimya.

“Rais Ramaphosa anajifanya kutoona yanayoendelea nchini Uganda. Kimya cha AU ni ishara kwamba wameafikiana na ukandamizaji dhidi ya viongozi wa upinzani unaoendelea humu nchini,” akasema Wine.

Akaongeza: “Rais Ramaphosa akemee ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelea nchini Uganda. Hata Uganda ilisimama na raia wa Afrika Kusini wakati wa ukandamizaji wa wakoloni. Tunaomba Ramaphosa na AU kusimama nasi; kusimama na watu wa Uganda na kuhakikisha kuwa demokrasia inazingatiwa.”

Alisema kuwa hakuna kiongozi wa EAC na AU amejitokeza kukemea vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa kampeni nchini Uganda.

You can share this post!

RIZIKI: Funzo la Covid-19 katika suala la ajira

SHINA LA UHAI: Hofu ya makali ya virusi vipya vya corona