Habari Mseto

Bodaboda Mwihoko waandamana baada ya vibanda vyao kubomolewa

June 23rd, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAENDESHAJI bodaboda eneo la Mwihoko, Githurai, waliandamana wakidai Kaunti ya Kiambu inawadhulumu kwa kubomoa vibanda vyao vya kujikinga jua kali na mvua.

Walidai ya kwamba mnamo mwishoni mwa wiki katika usiku wa manane, watu waliokuwa na magari ya kaunti hiyo walifika na kubomoa vibanda hivyo.

“Miezi michache iliyopita mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alijengea wahudumu vibanda kadha katika eneo hili, lakini viongozi wengine wasiotaka maendeleo wanajaribu kuvibomoa,” alisema kiongozi wa vijana eneo hilo Bw Mwangi Mwiheko.

Alitoa madai kwamba kuna baadhi ya viongozi wachache Kiambu ambao hawataki kuona wenzao wakisaidia vijana.

Wahudumu hao walisema wanaendelea kutetea haki yao hadi matakwa yao yatimizwe.

“Vijana ndio wanapitia masaibu mengi kwa sababu hawana ajira na kwa hivyo hawatakubali mara hii kugawanywa kama hapo awali,” alisema Bw Mwiheko.

Mwendeshaji bodaboda eneo la Mwihoko Bw Stephen Kimemia, alisema waliotenda kitendo hicho ni watu ambao hawataki maendeleo ya vijana bali wanataka kujinufaisha kisiasa.

Wahudumu wa bodaboda wa Mwihoko, Githurai wakiandamana Juni 19, 2020, baada ya vibanda vyao vya kujisitiri jua kali na mvua kubomolewa. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema uchunguzi unastahili kufanywa ili kubainisha hasa ni watu gani waliotenda kitendo hicho alichokitaja ni cha uhuni.

Alisema vijana kwa sasa wako tayari kupokea misaada kutoka kwa kiongozi yeyote ikiwa hata atatokea ama Mombasa, Kisumu au Nairobi.

“Sisi kama vijana wa Mwihoko na maeneo mengine hatutakubali kugawanywa na viongozi wachache kwa wanufaa yao wenyewe,” alisema Bw Kimemia.

Alisema kwa sasa wameachwa katika hali ngumu kwani mvua inayoendelea kunyesha inaponza juhudi zao za kufanya kazi.

“Tunaomba wahisani popote walipo wajitokeze ili kutujali sisi wahudumu wa bodaboda,” akaongeza.