Bodaboda sasa wapumua msako ukisimamishwa

Bodaboda sasa wapumua msako ukisimamishwa

JURGEN NAMBEKA na WINNIE ATIENO

WAENDESHAJI wa bodaboda wamepata afueni baada ya polisi kusitisha msako uliotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mapema wiki hii.

Msako huo ulizua mdahalo mkali wanasiasa wakilaumu serikali kwa kuchukulia wanabodaboda wote kama wahalifu.

Rais Kenyatta aliamuru msako huo baada ya wanabodaboda kadhaa, kumdhulumu na kumwibia simu mwanamke afisa wa ubalozi katika barabara ya Wangari Maathai, Nairobi.

Kitendo hicho kilikashifiwa vikali na viongozi, wanaharakati na Wakenya kwa jumla wakiwalaumu wahudumu wa bodaboda kwa kuchukua sheria mkononi.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i aliapa kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuwataka waendeshaji pikipiki kusajiliwa upya na idara husika.

Jana Jumamosi polisi, kupitia taarifa walisema kwamba msako huo utasitishwa kwa muda ili kuruhusu mazungumzo.

“Msako tulioanzisha wiki jana tukitaka kuweka sawa sekta ya uchukuzi wa umma haswa bodaboda, kwa sasa tumeusitisha. Tunataka tupange upya sekta hii, kwa kujadiliana na washikadau kutoka sekta mbalimbali kupitia kamati spesheli,” alisema Inspekta Mutyambai.

Polisi walikuwa wamekamata maelfu ya pikipiki na waendeshaji waliokiuka sheria za trafiki.

Wanasiasa nao walijiunga na wanabodaboda hao kulalamikia msako huo wakisema hata wale wasio na makosa walikuwa wakinyanyaswa.

Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga alitoa wito kwa polisi kuwasaka na kuwakamata wahalifu wanaojificha katika sekta ya wahudumu wa bodaboda badala ya kukamata kila mtu katika sekta hiyo kwani si wote ni wahalifu.

“Kuna wengine ambao wanamiliki pikipiki na hata hawako katika biashara. Watu kama hao hawafai kuhangaishwa,” akasema Bi Wanga.

Katika Kaunti ya Homa Bay, zaidi ya pikipiki 40 zimekamatwa jambo linalowafanya baadhi ya wamiliki kushindwa kujikimu.

Nao waendeshaji bodaboda kaunti ya Mombasa walikuwa wameisihi idara ya usalama kutomaliza biashara yao wakisema watafuata sheria.

Wakiongea kwenye mkutano wa kujadili usalama kwenye sekta ya bodaboda, wahudumu hao waliapa kushirikiana na vyombo vya usalama kudumisha usalama.

Mshirikishi wa bodaboda kaunti ya Mombasa Bw Martin Oyoo aliomba msamaha kwa wanawake wakiapa kushirikiana na polisi kuweka usalama.

“Kuna wahalifu kwenye sekta hii lakini wengi wetu tuko kazini na tumesajiliwa. Tunaomba serikali ikabiliane na wahalifu kwenye sekta hii. Sisi tunaweza kutambua wahalifu ndio maana tumeweza kuwakamata na kuwapeleka kwa kituo cha polisi,” alisema Bw Oyoo.

Msako huo uliathiri shughuli za uchukuzi huku wengi wa wanabodaboda wakilalamikia kuhangaishwa na kudhulumiwa na polisi waliokuwa wakiutekeleza.

Ghasia zilizuka katika baadhi ya maeneo wanabodaboda wakikabiliana na polisi.

Hata hivyo, baadhi ya wanabodaboda walijitosa mitandaoni kuomba msamaha wakisema wako tayari kutimiza mahitaji na kuzingatia sheria.

You can share this post!

Ruto apata tikiti ya UDA kuwania urais

PENZI LA KIJANJA: Asiyekufaa kwa dhiki, ni tapeli wa mapenzi

T L