Habari Mseto

Bodaboda wagombania ‘zawadi’ ya Uhuru ya Sh3 milioni

October 26th, 2020 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

SIKU chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwatunuku wanabodaboda wa Kaunti ya Kisii kima cha Sh3 milioni ili wagawanye miongoni mwao, baadhi ya wahudumu wamejitokeza na kudai walipunjwa hela hizo na viongozi wanaowasimamia.

Baada ya kuliongoza taifa kuadhimisha sherehe za Mashujaa katika uga wa michezo wa Gusii Jumanne wiki iliyopita, Rais Kenyatta pamoja na kinara wa ODM Raila Odinga walikutana na wahudumu hao siku iliyofuatia na kuwapa msaada huo.

Kwa kuwa idadi ya wahudumu waliohudhuria mkutano huo ilisemekana kuwa watu 3,000, kila mmoja alitazamia kupokea angalau Sh1,000 lakini hilo halikufanyika.

Kulingana na wahudumu wa steji ya Capital; inayopatikana katikati mwa mji wa Kisii, wengi wao walipokea Sh200, kiasi ambacho ni cha chini mno.

Sasa bodaboda hao wameibua maswali kulikoenda pesa zingine na kutaka majibu ya haraka.

“Rais mwenyewe alituuliza kama tunataka pesa tugawane au azitume kwenye hazina yetu ya akiba. Wengi wetu tulisema tupewe pesa hizo tugawane kwani tunaelewa vyema zikienda kwenye akiba zitaliwa na wachache ili wajifaidi wao binafsi. Hata baada ya kila mmoja kujua atapokea ngapi bado hela hizo zimepotea. Ikiwa za kugawana zimeliwa, sembuse zingepelekwa kwenye akiba ambapo ni watu wachache huzidhibiti,” akasema Bw Denis Maikuri, mmoja wa wahudumu.

Sasa, bodaboda hao wameiomba serikali ya kaunti kuwasaidia kufanya uchunguzi wa kulikoenda hela zingine na iwapo itang’amuliwa pesa hizo zilifujwa, wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia, wahudumu hao wameomba usimamizi wa gatuzi hilo kufanya kila wawezalo kuhakikisha uchaguzi wa wanabodaboda ambao umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara umefanyika haraka iwezekanavyo ili kuwaondoa afisini viongozi fisadi.