Bodaboda wahalifu wadhibitiwe haraka

Bodaboda wahalifu wadhibitiwe haraka

Si jambo geni kwamba wahudumu wa bodaboda humu nchini wamekuwa kero kubwa.Hii ni sekta ambayo imewapa vijana ajira na matumaini ya kukimu maisha yao kwa njia halali.

Hata hivyo, kuna wale ambao wanatumia fursa hii kuendeleza uhalifu kwa ujasiri wa ajabu, mijini na vijijini. Matukio mengi ya uhalifu yanayoripotiwa aghalabu hutokana na bodaboda wahalifu.Tukio la hivi majuzi lililovuma mitandaoni – ambapo afisa wa polisi alionekana akipokonywa simu aliyokuwa akipiga – ni ithibati tosha kuwa sekta hii ya uchukuzi inahitaji mikakati mahususi kudhibiti wahalifu tele walioivamia.

Ikiwa walinda usalama wenyewe ndio hao wanaibiwa simu na kutendewa visanga vingine mchana peupe, sembuse raia wa kawaida? Ni wazi kwamba hakuna yeyote aliye salama; si mijini, vijijini. Wanabodaboda wahalifu wanafaa kudhibitiwa mara moja kwa njia itakayopunguza uhalifu wanaoendeleza.

Wamezidi kwa wizi wa simu na vibeti vya kina dada barabarani, na pia huvamia mwendesha gari yeyote atakayekinzana nao. Mara nyingi vijana hawa huwa wamefanya makosa, lakini kwa vile ni wengi wanawavamia madereva kwa kila aina ya silaha ili kumlinda mwenzao.

Siku hizi si rahisi kujua bodaboda halali na mhalifu.Hivyo, mamlaka za usalama nchini zinapaswa kuhakikisha wahudumu hawa wote wanajiunga na vyama vya ushirika, kama ilivyo desturi katika sekta ya matatu.

Kisha wapewe mafunzo ya uendeshaji pikipiki katika vyuo anuwai vinavyotoa mafunzo kama hayo. Vibandiko vinapaswa kuwekwa kwenye pikipiki zao ili kuonyesha iwapo wana leseni, wamepata mafunzo wapi na vyama vya ushirika walivyojiunga navyo.

Pia, nambari za usajili za kila bodaboda ziwekwe mahali pake, na zionekane kwa wazi kabisa.Wanahitaji pia mafunzo ya usalama barabarani na namna ya kutumia barabara zao ipasavyo, na kwa kuzingatia usalama wa watumiaji wengine.

Kubuniwe pia kitengo cha polisi kitakachofuatilia wahalifu wanaotumia pikipiki; haswa miongoni mwa bodaboda na kuwatia mbaroni iwapo watahepa. Mikakati hii ikiwekwa, tutakuwa na utulivu barabarani navyo visa vya uhalifu vitapungua kwa asilimia kubwa.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa Jubilee wasipuuze maoni...

Raila amtaka Rais afungue nchi sasa