NA RICHARD MUNGUTI
SERIKALI Jumanne imevuna Sh7 milioni kufuatia kushtakiwa kwa wahudumu wa bodaboda wapatao 200 walioshtakiwa kwa makosa mbalimbali katika mahakama ya Milimani, Nairobi.
Wahudumu hao walitiwa nguvuni kufuatia agizo la Serikali wasakwe na kukamatwa kwa kukaidi sheria za trafiki.
Kila mmoja wa wahudumu hao alitozwa faini ya Sh35,000 na hakimu mwandamizi Bi Esther Kimilu.
Wahudumu hao wa bodaboda walikiri mashtaka ya kuvunja sheria za trafiki kwa kuendesha pikipiki kando ya barabara na kuzuia magari na waendao kwa miguu kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao walikiri mbele ya hakimu mwandamizi Bi Esther Kimilu kwamba walikiuka sheria za barabara.
Wahudumu hao waliomba msamaha wakisema “hawatarudi kukiuka sheria za trafiki tena.”