Habari za Kaunti

Bodaboda waliochukuliwa wapachikaji mimba wawalinda wasichana Kilifi

January 5th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

JAMII imetakiwa kuwapa nafasi sawa watoto wa jinsia zote ili kuhakikisha taifa la kesho linapiga hatua kimaendeleo, hususan kwa kuwapa nafasi wasichana ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto za ndoa za mapema na mimba za utotoni.

Kulingana na naibu gavana wa Kaunti ya Kilifi Bi Florence Mbetsa Chibule, jinsia zote mbili zina uwezo wa kuongoza taifa, na ni sharti wazazi wakubali kuwa jinsia zote ziko sawa na zinahitaji kupewa nafasi sawa katika jamii ili kufikia viwango vya juu zaidi.

“Tuko nao wasichana wetu na tunataka kutoa wito ya kwamba wasichana wetu walindwe, tumekataa mimba za mapema, tumekataa ndoa za mapema. Tunasema tuipe kila jinsia nafasi ya kujenga nchi kwa sababu kila jinsia ina uwezo wa kufika mbali. Vijana wetu mpaka lazima tuwalinde,” alisema Bi Chibule.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Bi Florence Mbetsa Chibule akiwa ameshika jezi yenye ujumbe ‘Zuia Mimba za Mapema’. PICHA | ALEX KALAMA

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, Bi Chibule ameeleza kufurahishwa kwake kutokana na mradi wa Linda Dada ambao unahusisha vijana wa sekta ya bodaboda kuwa katika mstari wa mbele kuwalinda wasichana wadogo walioko shuleni.

“Mheshimiwa Gavana, tunashukuru kwa sababu ulianzisha huu wito wa Linda Dada, ambao vijana wetu wa bodaboda wameuchangamkia kuhakikisha wasichana wanalindwa dhidi ya gumegume. Na sisi wazazi tulinde watoto wetu wa kike na wale wa kiume,” akasema.

Pia aliwashukuru viongozi wa kidini ambao kwa njia moja au nyingine wameweza kuwashauri hao vijana kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa katika jamii.

Kwa muda mrefu vijana wa sekta ya bodaboda wamekuwa wakisemekana kuwatunga mimba wasichana wa shule.

Lakini sasa wako katika mstari wa mbele kuripoti visa vya wale ambao wanakiuka sheria kwa kufanya mapenzi na watoto wa shule.