Bodaboda wapiga teke punda Lamu

Bodaboda wapiga teke punda Lamu

Na KALUME KAZUNGU

WAMILIKI punda katika Kaunti ya Lamu wanazidi kujawa na wasiwasi kuhusu hatima ya biashara yao ya uchukuzi, baada ya wateja wao wengi kugeukia usafiri wa bodaboda.

Sekta ya punda ndiyo njia kuu ya usafiri Lamu tangu jadi, ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wakazi huishi maeneo ambayo ni visiwa na hivyo ni vigumu kutumia mbinu nyingine ya uchukuzi kama vile magari.

Zaidi ya punda 10,000 wanapatikana katika Kaunti ya Lamu, idadi kubwa ikiwa ni wale wanaotumika kusafirisha watu na mizigo kwenye visiwa vya Lamu, Pate, Kizingitini, Faza, Siyu, Ndau, Mkokoni, Kiwayu na Kiunga.

Katika kikao na wanahabari mnamo Ijumaa, wamiliki punda walieleza haja ya wao kuunda chama chao halisi kitakachosaidia kupigania haki zao za kimsingi.

Bw Omar Kidege alisema biashara ya pikipiki katika kisiwa cha Lamu imekuwa kero kwao huku wengi wakinyang’anywa abiria na wahudumu wa bodaboda.

Karibu wahudumu 300 wa bodaboda wanapatikana Lamu licha ya kuwa, kisheria usafiri wa pekee unaokubalika ni ule wa miguu, punda au mikokoteni ili kuhifadhi desturi za mji huo wa kale.

Bw Kidege alisema yamkini wenye punda wangekuwa na chama chao, kingekuwa tayari kimejitokeza kupigania biashara yao ambayo inaendelea kumenywa na wenye pikipiki.

“Kila kukicha tunasukumwa nje ya soko na hawa bodaboda ambao wanaendelea kutawala uchukuzi ndani ya Lamu. Chama pia kitatuwezesha kupata mikopo ili kuinua zaidi sekta yetu,” akaeleza Bw Kidege.

Kwa upande wao, wahudumu wa bodaboda walijitetea kwamba huduma zao zimesaidia kupunguza idadi ya vijana wanaotumia mihadarati na kutekeleza uhalifu mitaani.

Kupitia mwenyekiti wao, Bw Abubakar Yusuf Abdallah, walisema tayari wameleta mabadiliko kwani wanaweza kupeleka mizigo maeneo ya mbali ambayo ni vigumu kufikiwa kwa kutumia punda au mikokoteni.

Hivyo, waliwataka wenzao wanaoendesha biashara ya usafiri kwa punda na mikokoteni kushirikiana nao ili kila mmoja apate riziki.“Wamiliki punda na mikokoteni waache kulalamika. Kuna baadhi ya kazi tunawaachia; sisi hufanya sana kazi za kusafirisha mizigo na wateja sehemu za mbali, hasa nje ya Lamu,” alihoji Bw Abdallah.

Bw Mohamed Ali ambaye ni mmiliki wa punda mtaani Bajuri alisisitiza kuwa haja yao kuunda chama ni kuwawezesha kuwasilisha malalamishi kwa serikali ya kaunti kwa urahisi ili yasikilizwe na kutatuliwa.

Alisema changamoto nyingine ambayo watafanikiwa kuwasilisha kupitia kwa chama ni kufariki kiholela kwa punda wao.Bi Fatma Athman alitaja kukosekana kwa mipangilio kabambe miongoni mwa wenye punda Lamu kama sababu kuu inayofanya haki zao kukiukwa kiholela.

Aliwataka kuzinduka na kubuni chama haraka iwezekanavyo ili wafaidi na mengi yanayotolewa serikalini.

“Chama hurahisisha upiganiaji wa haki miongoni mwa wanachama. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Na hii ndiyo sababu ni rahisi kwa wanachama wa mashirika au makundi kupata fedha serikalini ilhali sisi wenye punda tunabaki nyuma. Tuamke,” akasema Bi Athman.

You can share this post!

Uhuru awasha upya moto mkali ngomeni mwake

LEONARD ONYANGO: Rais aingilie kati, azime joto kali la...