Habari Mseto

Bodaboda wavuna mafuriko yakileta masumbuko na msongamano Thika Road

April 24th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

BARABARA ya Thika Superhighway ilikuwa na sura tofauti asubuhi Jumatano magari mengi yakikwama kwenye msongamano mkubwa.

Abiria walionekana wamesikitika kwa sababu ilikuwa bayana walichelewa kuwahi walikokusudia kwenda.

Haya yote yalisababishwa na masumbuko ya mafuriko baada ya mvua kubwa kuponda jiji la Nairobi na viunga vyake.

Huku abiria wakisikitika wafanye nini kuwahi kazini na shughuli nyingine za asubuhi, wanabodaboda waliona nafasi ya kuvuna pesa.

“Wenye pesa pandeni bodaboda sasa!” mhudumu mmoja wa bodaboda alisikika akiita abiria.

Nauli zilipanda zaidi ya maradufu kwa waliopendelea kusafiri halahala kwa pikipiki.

“Hatupati kazi nyingi vile za kuwabeba abiria, lakini ukipata moja ama mbili ni kama umebeba wateja wengi,” alikiri mhudumu wa bodaboda Patrick Lumbaso.

Abiria walilipa zaidi ya Sh200 kutoka eneo la Clay Works hadi Githurai ambapo kwa kawaida nauli huwa Sh20.

Changamoto hizi barabarani zilisababishwa na maji mengi kufurika barabarani eneo la Kahawa Sukari.

Baadhi ya magari yalibadilisha mkondo wa safari na kurudi yalikotoka.

 “Itabidi nifanye kazi nikiwa nyumbani leo. Siwezi kukubali gari langu libebwe na maji huko mbele,” alilalama Joseph Kinyua aliyekuwa anasafari kutoka Thika kuelekea jijini Nairobi.

Mengine yalitumia barabara mbadala ambazo zilikuwa afadhali kuepuka masumbuko ya mafuriko.

Sehemu ya Thika Road haikuwa na magari madereva wakiepuka kusafiria walipoarifiwa kulikuwa na maji mengi mbele yake kati ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Githurai.

Mvua kubwa imesababisha uharibifu sehemu tofauti za jiji la Nairobi zikiwemo Westlands, Runda, Mathare na Kasarani.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imetoa tahadhari kuwa hali itaendelea ikiwaomba wananchi wachukue tahadhari.