Habari

Bodi ya unyunyiziaji kukatiza kandarasi ya kampuni ya Israel katika mradi wa Galana-Kulalu

May 29th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BODI ya Kitaifa ya Unyunyiziaji (NIB) itatema kampuni moja kutoka Israel iliyopewa kandarasi ya kutekeleza mradi wa kilimo cha unyunyiziaji wa Galana-Kulalu licha ya mradi huo kufyonza Sh6.1 bilioni.

Kwenye taarifa iliyotuma kwa Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, bodi hiyo inasema kuwa itaipiga teke kampuni ya Green Arava Ltd na kutoa kandarasi kwa kampuni zingine ili ziweze kukamilisha mradi huo. Kazi iliyosalia inakadiriwa kugharimu Sh989.5 milioni.

NIB imeiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Embu Njeru Ndwiga kwamba imeanzisha mchakato wa kuipokonya kampuni hiyo kazi kutokana na mvutano ya kila mara iliyopelekea kazi kukwama katika mradi huo Septemba mwaka jana.

“Bodi hii imeandika barua kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) na Hazina ya Kitaifa ikisaka maoni kuhusu pendekezo hili la kukatiza zabuni iliyopewa Green Arava Ltd. Na ripoti imetayarishwa na kundi la maafisa kutoka afisi ya AG, Hazina ya Kitaifa, Idara ya Unyunyiziaji na NIB kuhusu mwelekeo utakaofuatwa. Ripoti hiyo imewasilishwa kwa Waziri wa Kilimo,” ikasema taarifa hiyo.

Mradi huo, ambao awali ulipangiwa kugharibu Sh17.5 bilioni, ulianzishwa mnamo 2014 baada ya uzinduzi wake kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Ulilenga kukuza mahindi katika shamba la ekari 10,000 huku ikikadiriwa kuwa ekari moja ingezalisha magunia 40.

Ulipangiwa kukamilika mnamo Oktoba 2016 lakini kazi ilicheleweshwa kutokana na vuta nikuvute iliyotokea kati ya bodi ya NIB na kampuni hiyo ya Israel iliyopewa kandarasi hiyo kutokana na maelewano kati ya taifa hilo na Kenya.

Na mwaka wa 2017, mradi huo uliweza kuzalisha chini ya magunia 30 ya mahindi kwa ekari moja.

Kiwanda

Baadaye serikali kupitia NIB ilipunguza thamani yake hadi Sh7.2 bilioni kwa kufutilia mbali ujenzi wa miundo mbinu mingine kama vile kiwanda cha kusaga mahindi.

Hatua hiyo iliyeyusha lengo la awali la mradi huo la kuhakikisha kuwa bei ya unga wa mahindi inashuka hadi kati ya Sh50 na Sh60 kwa pakiti moja ya kilo mbili.

Wiki jana wasimamizi wa NIB na wakuu wa kampuni wa Green Avara walifika mbele ya kamati hiyo ya Seneti kuhusu Kilimo kuangazia changamoto inayoukumba mradi huo.

Baada ya wao kulaumia kwa muda, mwenyekiti wa Kamati hiyo Seneta Ndwiga aliamuru kwamba Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko afanye ukaguzi wa mradi huo tangu 2014 hadi sasa.

Afisi ya Bw Ouko ilipewa makataa ya siku 30 kukamilisha uchunguzi huo na kuwasilisha ripoti kwa kamati hiyo, ripoti itakayotoa mwelekeo kuhusu namna ya kufufua mradi huo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na magavana Amason Kingi (Kilifi) na mwenzake wa Tana River Dadho Gadhana ambao mradi huo unatekelezwa katika kaunti zao.