Habari Mseto

Bodi yapendekeza kuwe na baa 3,000 pekee Nairobi

April 2nd, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

JIJI la Nairobi huenda likawa na baa 3,000 pekee iwapo mapendekezo ya bodi ya kudhibiti uuzaji wa mvinyo yataidhinishwa na bunge la kaunti kuwa sheria.

Mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasilishwa na bodi katika bunge la Kaunti katika muda wa miezi miwili ijayo.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Bajeti ya Kaunti Jumatatu, naibu mkurugenzi wa Bodi ya Kutoa Leseni kwa Wauzaji wa Mvinyo Hesbon Agwena, alisema sera hizo zinalenga kukabiliana na ongezeko la baa jijini Nairobi.

Bw Agwena aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Bw Robert Mbatia alisema kuwa sera hiyo pia imependekeza idadi ya baa zinazofaa kuwa katika kila mtaa.

Naibu Mkurugenzi alisema kuwa bodi hiyo ilipoanza shughuli zake mnamo Novemba 2014, kulikuwa na baa 7, 200 zilizoidhinishwa.

“Lakini sensa tuliyofanya baadaye ilibaini kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya baa zilizokuwa zikihudumu bila leseni,” akasema.

Alisema kuwa ripoti ya sensa iliyofanywa mnamo 2016, ilionyesha kuwa jiji la Nairobi lilikuwa na jumla ya baa 12,500.

Kwa mfano, Bw Agwena alisema, Katikati mwa Jiji la Nairobi kuna jumla ya baa 2, 000 lakini ni 736 zilizoidhinishwa na serikali ya kaunti.