Makala

BOERA BISIERI: Lengo ni kumfikia Taraji Henson wa Hollywood

March 18th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KUTANA naye Boera Bisieri anayependa kutazama filamu za mwigizaji wa Hollywood, Taraji Penda Henson mzawa wa Marekani ambapo amepania kufikia kiwango chake maana humtia motisha zaidi.

Anasema Wakenya wanafanya vizuri katika uigizaji wanaelekea kuwapiku wenzao wa Nollywood japo waliwatangulia.

”Mwaka 2017 nilishiriki filamu iitwayo ‘On Your Marks’ iliyofaulu kuingia nusu fainali kwenye shindano la Miami Film Festive,” alisema na kuongeza filamu hiyo iliashiria anaweza kufika mbali.

Dada huyu wa miaka 26, kando na uigizaji ni mwanamitindo, mwandishi pia anamiliki duka ya kurembesha wanawake vidole.

Binti huyu hufanya na kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) jijini Nairobi, anakojivunia kushiriki filamu kama Heaven’s Gate and Hell’s Flames ambayo huangazia injili ya Mungu.

Kwenye jitihada za kueneza injili ya Mungu kupitia filamu hiyo wamefaulu kuzuru nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, Rwanda na Uganda.

Je alijiunga na uigizaji namna gani? Mwanzo wa ngoma alikuwa akishiriki masuala ya drama akiwa shuleni. ”Nilifanikiwa kupokea mafunzo ya miaka miwili kuhusu uigizaji katika taasisi ya Talanta Academy,” alifunguka na kuongeza kuwa alipata nafasi hiyo baada ya kufanya vizuri katika majaribio alipomaliza elimu ya sekondari mwaka 2010.

Binti huyu ambaye anajulikana kama Joyline hushiriki filamu ambazo huonyeshwa kupitia vituo vya televisheni pia kwenye kumbi za kijamii.

Msanii Boera Bisieri anayejulikana kama Joyline. Picha/ John Kimwere

Anasema yupo katika harakati za kuachia filamu moja mwezi ujao kwa jina ‘Which Way Sir‘ iliyofanyiwa kazi na Two Funny Productions. Filamu hiyo itazinfuliwa Aprili 7, katika ukumbi wa Kenya National Theatre.

Anajivunia kuigiza filamu ya TV Series The Guinders (World of Mysteries) iliyopeperushwa kupitia Ebru TV.

Pia alishiriki ‘Kijakazi’ iliyorushwa kupitia Maisha Magic vile vile TV Series chungu mzima chini ya produsa Fred Omondi bosi wa hapa na kule. Kadhalika aliwahi kushiriki kipindi cha vichekesho cha House of Kawangware ambacho huonyeshwa KTN kati ya zingine.

Kama mwandishi huandikia jarida la dijitali liitwalo Artmatters.info. Huchambua vitabu vya michezo ya kuigiza pia habari za masuala ya kijamii.

Kama mwanamitindo amehusika katika picha za matangazo ya kibiashara na kampuni kadhaa ikiwamo Betin, Visacard, Safaricom-Tunukiwa na GoTV miongoni mwa zinginezo.

Anasema angependa kuigiza filamu itakayovumisha sekta ya burudani katika viwango vya kimataifa lakini bajeti ndiyo kizungumti.

”Kazi bora ya muziki pia uigizaji huhitaji gharama kubwa suala ambalo hutesa wengi wetu,” alisema na kuongeza serikali inastahili kubuni mkakati utakaosaidia sekta ya burudani kuinuka ili kutoa nafasi za ajira kwa wasanii chipukizi.

Alisema serikali inastahili kushirikiana na waigizaji ili kufahamu vizuri tansia ya filamu na kufadhili miradi zao.

Anaamini kuwa wasanii wa Kenya wakipata ufadhili wameiva kufanya kazi bora na kuvutia wananchi ambao hupenda filamu ya kigeni na kupuuzilia mbali kazi wazalendo.