Boga aachia ODM kibarua Msambweni

Boga aachia ODM kibarua Msambweni

Na SIAGO CECE

MWENYEKITI wa Shirika la Kustawisha Miundomsingi ya Maji Pwani, Bw Omar Boga, ametangaza hatawania kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi ujao.

Bw Boga alikuwa amewania ubunge katika uchaguzi mdogo uliofanyika Msambweni mwaka uliopita lakini akashindwa na Feisal Bader.Bw Bader alikuwa mgombeaji huru aliyeungwa mkono na Gavana Salim Mvurya pamoja na wanasiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Uchaguzi mdogo ulifanywa baada ya kifo cha Suleiman Dori, ambaye alichaguliwa kupitia ODM lakini aliasi chama kabla kufariki kwake. “Nina kazi ambayo nilipewa na serikali na hilo ni kuhakikisha wakazi wote wa Pwani wanapata maji safi. Sitawania kiti mwaka ujao, nitakuwa mtazamaji,” alisema katika mahojiano na Taifa Leo.

Uamuzi wake kutowania unamaanisha ODM italazimika kutafuta mgombeaji mwingine.Chama hicho kimepoteza wabunge wote kaunti hiyo kwani Mbunge wa Kinango, Bw Benjamin Tayari, pia aliasi chama. Bw Tayari ameashiria atatetea kiti chake kupitia United Democratic Alliance (UDA).

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti, Bi Zuleikha Hassan, ndiye sasa anatarajiwa kupeperusha bendera ya ODM katika eneobunge la Kinango mwaka ujao.Katika eneobunge la Matuga ambapo Chama cha Amani National Congress (ANC) ndicho kilishinda kupitia kwa Bw Kassim Tandaza mwaka wa 2017.,. mbunge wa zamani Hassan Mwanyoha anawania tikiti ya ODM.

Hakuna mwanasiasa amejitokeza kufikia sasa kuashiria amepanga kuwania ubunge Lungalunga kupitia kwa ODM.Kaunti hiyo ni mojawapo ya sita za Pwani ambazo zimevutia ziara nyingi za wanasiasa wanaopanga kuwania urais mwaka ujao.

Katika uchaguzi uliopita, Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga alipata kura nyingi eneo hilo kuliko zile za Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Wanyonyi Cup mechi 32 kuchezwa wikendi hii

Hofu Ukimwi ukisambaa kwa kasi miongoni mwa watumiaji...

T L