Siasa

Boga akanya Mvurya kuingiza vita vyake na Joho katika kampeni

November 28th, 2020 2 min read

Na FADHILI FREDRICK

MWANIAJI ubunge wa Msambweni kupitia chama cha ODM, Bw Omar Boga, amemtaka Gavana wa Kwale Salim Mvurya akome kutumia kampeni za uchaguzi huo kumalizana kisiasa na Gavana Hassan Joho wa Mombasa.

Akizungumza katika msururu wa mikutano ya kujipigia debe kabla ya uchaguzi mdogo wa Disemba 15, Bw Boga alisema kwamba Bw Mvurya alikihama chama cha ODM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2017, na kwamba hastahili kuingilia masuala ya chama hicho.

“Tunahitaji siasa za ukomavu Msambweni ambazo zitaangazia jinsi wakazi watakavyonufaika na uongozi bora. Si hizi siasa za kukashifiana. Si sawa kwamba Bw Mvurya kila aendako anaukashifu uhusiano wangu na Gavana Joho. Kama ana tofauti na Joho, wazitatue nje ya kampeni hizi. Joho ni naibu kinara wa chama chetu na hakuna vile ambavyo nikiwa mwaniaji kwa tikiti ya ODM nitakosa kushirikiana naye,” akasema Bw Boga.

Gavana Mvurya na naibu wake Bi Fatuma Achani, wamejitosa ulingoni waziwazi kumpigia debe mgombea wa kujitegemea Bw Feisal Bader, ambaye anaungwa mkono na Naibu Rais William Ruto na wandani wake.

Bw Boga na Bader ndio wanaopigiwa upatu kutoana kijasho katika kinyang’anyiro hicho, ambacho kimewavutia wagombea wengine sita. Mbali na wagombea huru Charles Bilali na Mansury Kumaka, kuna Hassan Mwakulonda (Party of Economic Democracy), Khamis Mwakaonje (United Green Movement), Shee Abudulrahman (Wiper) na Marere Wamwachai (National Vision Party).

Bi Mwachai aliyewahi kuwa mbunge wa eneo hilo, ndiye mgombea pekee wa kike aliyesalia katika kujipima nguvu na wanaume saba, baada ya mgombea huru Mariam Sharlet Akinyi kujiondoa na kuahidi kumuunga Bw Boga. Akizungumza hivi majuzi katika kijiji cha Mulungunipa akimpigia Bader debe, Bw Mvurya aliwarai wakazi wa Msambweni kutomchagua Bw Boga kwa dai kuwa yeye hashirikiani na viongozi wa kaunti hiyo.

“Kama yeye Boga hashirikiani na viongozi wa kaunti hii bali anashirikiana na viongozi wengine na kutonitambua mimi kama gavana, je kweli anaweza kujali nyinyi wananchi atakapopata uongozi?” akauliza.

Bw Mvurya aliwaomba wakazi wa Msambweni wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi na kumchagua Bw Bader, anayesema ana uzoefu kwa kuwa aliwahi kufanya kazi na marehemu Suleiman Dori, aliyefariki mwanzoni mwa mwaka huu.

“Msambweni tulimpoteza mbunge mchapa-kazi. Sote tuna huzuni na tutafarijika tukimpeleka Bader bungeni, ili aweze kuendeleza miradi ilioanzishwa na marehemu,” akasema.