Habari Mseto

Boinnet achukua hatua kuhusu ulinzi wa mhubiri Owuor

December 31st, 2018 2 min read

BENSON MATHEKA Na ERIC MATARA

Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet, alijitenga na ulinzi ambao mhubiri David Owuor alipatiwa na maafisa wa polisi hivi majuzi akisema walioruhusu Bw Owuor kupatiwa ulinzi huo mkali watachukuliwa hatua.

Bw Owuor mnamo Ijumaa aliwasili Nakuru chini ya ulinzi mkali akisindikizwa na msafara wa magari 40 na pikipiki za polisi.

Bw Boinnet alitaja hatua hiyo kama matumizi mabaya ya mali ya umma. “ Sheria inaruhusu mtu kukodi maafisa wa polisi kudumisha usalama kwenye hafla za kibinafsi, hata hivyo sio kwa kiwango ambacho (Owuor) alikuwa nao.

Hatua zitachukuliwa waliohusika. Kisheria, matumizi mabaya ya mali ya umma hayaruhisiwi,” alisema Bw Boinnet. Muda mfupi baada ya kauli ya Bw Boinnet, polisi mjini Nakuru waliyakamata magari matatu ya polisi aina ya Land Cruiser kutoka vituo vilivyo nje ya kaunti hiyo ishara kwamba baadhi ya maafisa waliokuwa kwenye msafara huo walitoka nje ya Kaunti ya Nakuru.

Kisheria, kwa sababu hafla ilikuwa Nakuru, ni maafisa kutoka eneo hilo waliopaswa kutumwa kudumisha usalama. Hii hufanyika mtu akituma ombi la kukodi maafisa wa polisi na ombi hili kukubaliwa.

Bw Boinnet alisema ingawa sheria inaruhusu mtu kukodi maafisa wa polisi kudumisha usalama wakati wa hafla za kibinafsi, hairuhusu mtu kuwa na idadi ya waliokuwa na Bw Owuor. “Idadi ( ya polisi waliomlinda Owuor) haifai, ni matumizi mabaya ya mali ya umma,” alisema Bw Boinnet.

Kulingana na Kamanda wa polisi Kaunti ya Nakuru Hassan Barua, magari hayo yalikamatwa kwa kupatikana mbali na vituo yanayopaswa kuhudumu bila idhini.

“Ni kweli polisi wanazuilia magari matatu ya polisi ambayo yalipatikana bila idhini ya kuwa nje ya vituo yanayopaswa kuhudumu. Yanazuiliwa katika makao makuu ya polisi eneo la Rift Valley,” alisema Bw Barua. Magari ya polisi, sawa na mengine ya serikali, yanapaswa kuhudumu maeneo yaliyotengewa na yanapaswa kutoka nje ya maeneo haya kwa idhini ya wakuu wa polisi na dereva kupatiwa barua kumruhusu kufanya hivyo. Hata hivyo, Bw Barua alikanusha kwamba magari hayo yalizuiliwa kwa kumsindikiza Bw Owuor.

Uchunguzi wa Taifa Leo uligundua kwamba, baadhi ya magari yalitoka vituo vilivyoko Kaunti za Nairobi na Tharaka Nithi. Bw Barua hakueleza walikokuwa madereva wa magari yaliyokamatwa akisisitiza yalikamatwa kwa sababu ya kuwa nje ya vituo vya kazi bila idhini.

Mnamo Ijumaa, Taifa Leo ilifichua jinsi Bw Owuor alivyowasili Nakuru kwa mkutano wa injili kwa mbwewe akilindwa kama mtu mashuhuri.