Kimataifa

Boko Haram waua watu 19 Nigeria

August 20th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

Wapiganaji wa Boko Haram, Nigeria usiku wa Jumapili waliripotiwa kuua watu 19 walipovamia kijiji kilichoko kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.

Wakiwa wamejihami kwa silaha kali wanamgambo hao wanasemekana kuvamia kijiji cha Malari mwendo was aa nane usiku na kutekeleza mauaji hayo.

Abatcha Umar ambaye aliokoka kifo alieleza shirika la Reuters kuwa alihesabu miili 19 ya watu waliouawa katika mavamizi hayo, japo mfanyakazi mmoja katika kambi iliyopokea manusura akisema waliokufa ni 63.

Mamia ya wakazi wa vijiji jirani na hicho sasa wametorokea katika kambi hiyo iliyoko mji wa Garrison, eneo la Monguno jimbo la Borno, wakasema wafanyakazi wa kambi hiyo.

Wapiganaji hao wanasemekana kuingia kijiji cha Malari jioni Jumamosi jioni wakitumia malori, wakipiga risasi na kurusha grinedi, wakasema wanakijiji.

Kulingana na Aisami Grema, mwanakijiji, polisi wanaolinda doria katika kijiji hicho hawakufanya lolote wakati wa mavamizi hayo.

“Hawakufanya juhudi zozote kukabiliana na wapiganaji hao wa Boko Haram,” Grema akaeleza AFP.

Mwanakijiji mwingine alisema wapiganaji hao walizunguka kijijini kwa saa mbili kabla ya kuondoka.

Ijumaa iliyopita, wakulima wanne waliuawa na wapiganaji wa kundi hilo, wakati lilipovamia mashamba karibu na eneo la Maiduguri.

Wanamgambo hao wamekuwa wakizidisha mavamizi hata kwa vikosi vya usalama, jambo ambalo limeonekana kuwa pigo kwa serikali ya nchi hiyo haswa uchaguzi wa Februari mwaka ujao unapoelekea.

Kundi la Boko Haram liliundwa katika eneo la Maiduguri mnamo 2002 na limekuwa likitumia fujo kupigaana na usemi wa mataifa ya magharibi katika nchi za magharibi mwa Afrika.

Adhari zake zinasikika mataifa ya Chad, Nigeria na Cameroon, hadi sasa likituhumiwa kuua zaidi ya watu 20, 000 na kusababisha zaidi ya watu milioni mbili kuhama makwao.