Michezo

Bolt ajaliwa mtoto wa kwanza

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MTIMKAJI Usain Bolt ambaye ni mshindi mara nane wa medali za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki na binadamu mwenye kasi zaidi duniani, sasa ni kidume kamili baada ya mchumba wake wa muda mrefu, Kasi Bennett, kujaliwa kimalaika cha kike.

Miongoni mwa watu maarufu ambao wamempongeza Bolt kwa baraka hiyo ni Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness aliyesema, “Hongera sana nguli wetu wa mbio za masafa mafupi, Usain Bolt na mwenzako Kasi Bennett kwa kujaliwa mtoto.”

Akitumia mtandao wake wa Instagram, Bolt, 33, alizianika habari hizo njema kwa mashabiki wake japo aliahidi kubana jina la mtoto wao kwa sasa.

Bolt ambaye ni mtimkaji wa pekee anayejivunia kuzoa nishani za dhahabu katika mbio za mita 100 na mita 200 katika Michezo ya Olimpiki kwa mara tatu mfululizo (2008, 2012, 2016), amesema kwa sasa anapania kufunga pingu za maisha mwishoni mwa mwaka huu na kupata watoto wawili zaidi.

Nyota huyo ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 100 na mita 200 mara 11, alistaafu rasmi mnamo 2017 baada ya kunogesha Riadha za Dunia jijini London, Uingereza.

Alijiunga baadaye na kikosi cha soka cha Central Coast Mariners nchini Australia mnamo 2018 kabla ya juhudi za kurasimisha mkataba wake kugonga mwamba.

Olimpiki za Tokyo, Japan mwaka ujao zitakuwa za kwanza tangu zile zilizoandaliwa jijini Sydney, Australia mnamo 2000 kukosa mbwembwe za Bolt ugani.

Habari za Bolt kula bata na Kasi zilifichuka mnamo 2016 jijini Rio, Brazil wakati wa Olimpiki ambapo Bolt alijiachilia na mademu wa kila sampuli akiwamo mwanamitindo wa Uingereza Erica Carvalho na Dina Terror ambaye ni mjane wa watoto wawili.

Licha ya Christine ambaye ni dadake Bolt kumtaka mwanariadha huyo mstaafu kufunga ndoa na Kasi, mama yao, Jennifer, amekuwa akimpendekezea Bolt kula yamini ya ndoa na kipusa msomi wa masuala ya uanasheria nchini Brazil, Jady Durate.