Michezo

Bolt ang'atuka baada ya klabu kudinda kumpa mamilioni aliyotaka

November 2nd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Ndoa ya muda kati ya nyota Usain Bolt na klabu ya Central Coast Mariners kutoka Australia imevunjika Ijumaa baada ya kambi ya mfalme huyo wa mbio fupi kushikilia kwamba anastahili kupewa donge nono.

Wakala wa Usain Bolt, Ricky Simms alitaka mteja wake apewe kandarasi ya Sh213.3 milioni, lakini ripoti zinasema kwamba klabu hiyo kutoka Ligi Kuu ilikuwa tayari kumpa asilimia tano pekee (Sh10.6 milioni) kwa sababu haikuridhishwa sana na talanta yake.

Mshikilizi huyu wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 100 (sekunde 9.58) na mita 200 (sekunde 19.19) amekuwa akifanyiwa majaribio na klabu hiyo kutoka Ligi Kuu tangu awasili mwezi Agosti. Alitumai kutimiza ndoto yake ya utotoni ya kuwa mwanakabumbu shupavu. Ziara hiyo ya Bolt, 32, ilipata umaarufu kote duniani. Iliongezeka hata zaidi pale alipofuma wavuni mabao mawili katika mechi ya Mariners ya kujiandaa kwa msimu mpya.

Mariners imeandikisha sare mbili za 1-1 dhidi ya Brisbane Roar na Melbourne City katika mechi zake mbili za kwanza katika Ligi Kuu ya Australia almaarufu A-League. Itamenyana na Adelaide United mnamo Novemba 4.