Habari za Kaunti

Boma la mpinzani wa Gavana Ken Lusaka lavamiwa

February 26th, 2024 1 min read

NA JESSE CHENGE

POLISI katika Kaunti ya Bungoma wanachunguza kisa ambapo kundi la majambazi wasiojulikana walivamia boma la mwanasiasa mmoja eneo hilo Jumatatu, Februari 26, 2024 na kufanya uharibifu wa mali.

Bw Zacharia Barasa, ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana Bungoma 2027, boma lake lilivamiwa na wahuni na lango kuteketezwa.

Kulingana na wanafamilia na baadhi ya wafuasi wa Bw Barasa, waliskia milio ya risasi kadhaa wakati wa shambulio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa mwanasiasa huyo, Martin Nyongesa, nduguye Barasa, alilaani tukio hilo akisema akihoji na njama ya kuzima ndoto zake kuwa gavana wa Bungoma 2027.

kuwa ni mkakati wa kisiasa wa kudhoofisha ndoto ya kaka yake ya kuwa gavana.

Watu wakitazama lango la boma ya Zacharia Barasa, mwanasiasa Bungoma, lililoshambuliwa na kuteketezwa na kundi la majambazi ambao hawajajulikana. PICHA|JESSE CHENGE

Barasa anamezea mate kiti hicho kilichoshikiliwa na Bw Ken Lusaka, kupitia tikiti ya chama cha DAP-K.

“Tunavyozungumza, Bungoma haina kiongozi wa kulinda maslahi ya raia wa kawaida. Ni kaka yangu Zacharia ambaye anakabiliana na maslahi ya watu na matukio kama haya yanataka kumzuia lakini hatutasita kushutumu serikali ya kaunti,” Nyongesa alisema.

Alisifia Barasa akisema amekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kupigania maslahi ya raia Bungoma, akirejelea kubomolewa kwa biashara katika mji wa Bungoma ambapo Barasa alisimama kidete na wafanyabiashara walioathirika.

Nyongesa anadai kuwa walioshambulia nyumba ya kaka yake ni watu wanaojulikana na kuomba polisi kuchukulia hatua za kinidhamu.

“Watu walioshambulia makazi ya Barasa na kuteketeza lango lake ni wale wanaoogopa hatua zake za kisiasa, kama wanataka kukabiliana nasi waje mchana si usiku,” Nyongesa akawaka.

Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Bungoma.

Tayari baadhi ya wanasiasa eneo la Magharibi mwa Kenya na maeneo mengine nchini wameanza kuandaa jukwaa la kuwania viti 2027.