Habari

Hillary Barchok aapishwa kuwa Gavana wa tatu wa Bomet

August 8th, 2019 2 min read

Na VITALIS KIMUTAI

HILLARY Barchok ndiye Gavana mpya wa Kaunti ya Bomet baada ya kuapishwa Alhamisi kufuatia kifo cha Dkt Joyce Laboso.

Anakuwa gavana wa tatu wa kaunti hiyo.

Naibu Rais Dkt William Ruto ni miongoni mwa viongozi mashuhuri waliohudhuria sherehe hiyo.

Safari yake katika ulingo wa kisiasa ilianza miaka mitatu iliyopita. Wakati huo, Hillary Barchok alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka bila kujua kwamba aliyekuwa Gavana marehemu Laboso na washauri wake kisiasa walikusudia kumteua awe mgombea mwenza baada ya kuamua kuwania ugavana akilenga tiketi ya Jubilee.

Miongoni mwa wasomi, ni Dkt Barchok ndiye aliibuka kama mtu bora.

Gavana wa Kaunti ya Bomet, Hillary Barchok. Picha/ Maktaba

Mtaalamu huyu wa Kemia na Hisabati alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Elimu na Nguvukazi katika Chuo Kikuu cha Chuka.

Pia alikuwa ni mwanachama wa Mamlaka ya Mapato ya Kustaafu (RBA).

“Tulipoenda kumtafuta tulitaabika sana na hata karibu tubebe bango. Tulipata kama yuko ziarani nje ya nchi kikazi,” alisema Edward Abonyo (mume wa marehemu Laboso).

Barchok mwenyewe anakiri alikuwa limbukeni katika siasa.

“Sikuwa na tajriba katika siasa, lakini nina bahati kushirikiana na mabingwa wa siasa,” anasema Dkt Barchok.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2017 Laboso alimshinda Isaac Ruto wa Chama Cha Mashinani (CCM) ambaye alikuwa Gavana wa kwanza wa Bomet.

Sasa Barchok ameahidi kufuata nyayo za Laboso ambaye alizikwa Jumamosi, Agosti 3, 2019.

Laboso alifariki baada ya kuugua saratani kwa miaka mingi. Mumewe alisema aligundulika kuwa na saratani mwaka 1991.

Dkt Barchok anasikitika kumpoteza “rafiki, mama, mhadhiri mwenzangu na mtu ambaye alipenda maisha ya utulivu yasiyo na vituko na sakata”.

“Licha ya  kwamba kiongozi wetu ametangulia mbele ya haki, tuna Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kaunti (CIDP) ambao tutaendelea kuufuata,” Barchok aliambia Taifa Leo na NTV kwenye mahojiano.

Alikuwa akishughulikia masuala ya kaunti muda wote ambao Laboso alisafiri kuenda Uingereza Mei 29, 2019. Laboso baadaye alienda India na aliporejea akawa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu zaidi katika Nairobi Hospital kabla ya kufariki.

Barchok ni shabiki wa Chelsea na timu ya taifa Harambee Stars.

Kabla ya kuapishwa alikuwa amesema suala la usawazishaji na kuhakikisha kila jinsia inainuka katika jamii ni mojawapo ya malengo aliyo nayo.

Julai 2019 Kaunti ya Bomet ilizindua mradi wa Kuku na Mama ambapo vifaranga 5,000 vilipeanwa kwa makundi ya kina mama 40,000 katika wadi 25 kuinua wakazi kiuchumi na vilevile masuala ya lishe.