Habari

Bomoabomoa zawaacha wakazi wa mtaa wa Pangani kwenye kijibaridi

July 16th, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO

WAKAZI waliokodisha nyumba za makazi katika mtaa wa Pangani walilazimika kulala nje kwa kijibaridi kikali Jumatatu usiku baada ya matingatinga ya Kaunti ya Nairobi kubomoa nyumba zao.

Wakazi wa mtaa huo wamesema matingatinga hayo yalifika mwendo wa saa tano na nusu usiku na kuanza kuvunja madirisha na milango wakati ambapo walikuwa usingizini.

Mkazi mmoja ameelezea jinsi ambavyo tukio hilo la kutisha liliendelezwa wakati wangali nyumbani na watoto.

“Watu kutoka City Hall wako hapa wakiendeleza ubomozi; hali ni ya kutisha,” mkazi mmoja wa kike aliambia Taifa Leo.

Wakodishaji walilazimika kuondoka na kuelekea maeneo salama.

Mtaa wa Pangani pamoja na mingine sita, imeorodheshwa kwa ukarabati wa kuinua hadhi kwa ujenzi wa makazi bora zaidi.

Mitaa mingine jijini Nairobi ni Ngong Road Phase I na II, Uhuru Estate, New Ngara, Old Ngara, Suna Road, na Jeevanjee.