Habari

'Bomu' lavuruga shughuli JKIA

April 17th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

ABIRIA mmoja Jumatano alikamatwa na polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kueneza uwongo kwamba kulikuwa na bomu katika ndege moja iliyokuwa ikielekea Johannesburg, Afrika Kusini.

Madai hayo yaliibua hofu na kupelekea ndege hiyo ya Shirika la Kenya Airways (KQ) kusitisha safari  yake na uwanja huo ukafungwa kwa muda kufutia taharuki iliyotanda baada ya habari hizo kusambaa.

Polisi walisema kuwa purukushani ilitokea baada ya mabishano yaliyotokea kati ya abiria huyo na mhudumu wa ndege.

Inadaiwa kuwa abiria huyo alitaja jina, “bomu” wakati wa mabishano hayo, hali iliyowatia woga abiria ndani ya ndege hiyo ambayo ilikuwa tayari kuanza safari.

Hii ilimlazimisha rubani kusitisha safari huku mwanamume huyo akikamatwa na kuwasilishwa kwa polisi kwa mahojiano.

Kisa hiki kilipelekea kufungwa, kwa muda, kwa uwanja wa JKIA kutoa nafasi kwa polisi kuendesha upekuzi ulioendelea kwa saa kadha majira ya alasiri.

Abiria wengi walioathirika na hali hiyo walichapisha  gadhabu zao kwa mitandao ya kijamii wakilaani kucheleweshwa kwa safari zao

“Nawasikitikia watu wanaosafiri kwa ndege kutoka JKIA haswa kwa kutumia ndege ya KQ au Jambo Jet. Wamecheleweshwa kwa zaidi ya saa tatu kutokana na sababu za “kiufundi”. Sasa JKIA imefungwa kwa muda, na hali ni mbaya hata zaidi,” akasema abiria kwa jina Abbey, kupitia Twitter.

Ndege nyingi ambazo zilipanga kutua JKIA zilielekezwa katika viwanja vingine, haswa ule wa kimataifa wa Moi, Mombasa.

Hali ilirejea kawaida  katika uwanja huo wenye shughuli nyingi, mwendo was aa kumi na nusu jioni.