HabariSiasa

Bondi ya Sh30 milioni kwa Sonko

December 11th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ameachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu au bondi ya Sh30 milioni baada ya kushtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Akitoa uamuzi wa wake, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Douglas Ogoti pia aliamuru kwamba Govana Sonko na maafisa wengine wa kaunti ya Nairobi walioshtakiwa pamoja wazuiliwe kutekeleza majukumu ya afisi zao hadi kesi dhidi yao itakaposikizwa na kuamuliwa.

Hakimu huyo amerejelea amri iliyotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Mumbi Ngugi ambayo imewazuia Magavana Ferdinand Waititu (Kiambu) na Moses Lonolkulal (Samburu) ambao pia wanakabiliwa na kesi za ufisadi.

Gavana Sonko alifika kortini kwa ambulansi kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ambako alikuwa akipokea matibabu kutokana na majeraha aliyodaiwa kupata alipopambana na polisi wakimtia mbaroni Voi, Ijumaa.

Amri ya Hakimu Ogoti ya kumzuia Bw Sonko kurejea afisi sasa inamaana kuwa kuna ombwe la uongozi katika kaunti hiyo ikizingatiwa kuwa hajateua Naibu Gavana tangu Januari 2018, Polycarp Igathe alipojiuzulu.