Bondia Ajowi kutetea hadhi ya Hit Squad

Bondia Ajowi kutetea hadhi ya Hit Squad

GEOFFREY ANENE na CHARLES ONGADI

Mabondia Elly Ajowi, Martin Oduor na Joseph Shigali wanatumai kutetea hadhi ya Kenya kwenye Ndondi za Dunia jijini Belgrade, Serbia leo mambo yanapoendelea kuonekana kuwa magumu baada ya Wakenya watano kupanguliwa katika siku mbili ziliopita.

Boniface Mogunde alilemewa na raia wa Albania Alban Beqiri kwa alama 5-0 katika uzani wa kilo 71 hapo jana na kuungana wanamasumbwi wengine kutoka timu ya Kenya maarufu kama Hit Squad kuwa mashabiki.

Wengine waliokuwa wamebanduliwa wakati tulienda mitamboni ni David Karanja (kilo 51), Victor Odhiambo (kilo 63.5), Cosby Ouma (kilo 81) na Joshua Wasike (kilo 91).Ajowi, ambaye alikuwa kwenye Olimpiki 2020 miezi miwili iliyopita, atazichapa dhidi ya Jakhon Qurbonov kutoka Tajikstan katika uzani wa zaidi ya kilo 91.

Anarejea kwenye mashindano ya dunia baada ya kushiriki makala ya 2009 na 2013 alipobanduliwa mapema.“Nashukuru Mungu, Shirikisho la Ndondi Kenya (BFK) na serikali yetu kwa kutuwezesha kufika hapa.

Nitachukua pigano langu dhidi ya raia huyo wa Tajikistan litakavyokuja. Sote tuko hapa kushinda na sina hofu kuhusu uamuzi wa majaji,” alisema Ajowi hapo jana.Oduor aliomba Wakenya wamweke kwenye maombi akisema kuwa ana imani atalima raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Nathan Lunata katika uzani wa kilo 57.

“Sitaki hata kutafuta mitandaoni kujua uchezaji wake. Acha mikono itembee ulingoni,” alisema Oduor.Shigali alikuwa mwingi wa matumaini atamdengua Marco Hernandez kutoka Mexico katika uzani wa kilo 67.

“Hakuna bondia mnyonge hapa, lakini naenda kumfanyisha kazi ngumu mpinzani wangu,” aliapa Shigali.Aidha, Mogunde alieleza kushangazwa na uamuzi wa majaji kumtawaza Beqiri mshindi wa kilo 71.

“Nilijua niko mbele katika raundi ya kwanza na raundi ya tatu, ingawa sikuwa nimefanya vyema katika raundi ya pili. Hata hivyo, siamini kuwa nimepoteza pigano hili. Yote namwachia Mungu,’ alisema Mogunde.

You can share this post!

Sudi alitumia vyeti feki kuingia serikalini, mahakama...

LEONARD ONYANGO: Utafiti kuhusu hatari ya Ziwa Victoria...

T L