Michezo

Bondia Anthony Joshua azoa Sh2 bilioni kwa kumlima Povetkin

September 24th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Bondia Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua alivuna Sh2, 649,927,401 kwa kumlima Alexander Povetkin katika dakika ya 19 na sekunde 59 ya pigano la dunia la mataji ya uzani wa WBA (Super) na IBF, WBO na IBO (Heavy) uwanjani Wembley jijini London, Uingereza mnamo Septemba 22, 2018.

Muingereza huyu alihakikisha majaji hawahitajiki kuamua mshindi dhidi yake na Mrusi Povetkin, ambaye hakuwa mchache.

Mbele ya mashabiki 80,0000 uwanjani Wembley, Joshua alitikiswa katika raundi za mwanzo. Povetkin, 39, ambaye alijishindia Sh794, 818,921, alionyesha Joshua hakuwa Uingereza kutalii alipomfanya apepesuke katika raundi ya kwanza baada ya kumsukumia ngumi nzito ya kulia kwenye kidevu na kumuongeza ya kushoto.

Ingawa Joshua hakutatizwa sana na mbinu za Povetkin, alimaliza raundi hiyo akitokwa na damu puani. Mrusi pia alianza raundi ya pili vyema kabla ya Joshua kujaribu kurejea kwenye mechi. Alimpa Joshua tumbo joto katika raundi ya tatu pale alipomrushia ngumi nzito ya mkono wa kushoto baada tu ya kumsukumia ngumi na mkono wa kulia.

Hata hivyo, Povetkin alianza kuona vimulimuli katika raundi ya nne aliposukumiwa ngumi kwenye nyusi zake za jicho la kushoto, alama ambayo ilimpa Joshua matumaini. Ngumi nyingi za Povetkin katika raundi ya tano na sita hazikumpata Joshua, huku Muingereza huyu akiendelea kujiamini kutokana ushabaha wake mwenyewe. Joshua, 28, alimaliza kazi katika dakika ya kwanza na sekunde 59 ya raundi ya saba kwa kumrushia Povetkin mvua ya ngumi.

Aliangusha Mrusi huyu sakafuni mara mbili katika raundi hii kabla ya refa Steve Gray kuamua kusimamisha pigano kuokoa Povetkin. Baada ya pigano hili, Promota wa Joshua, Eddie Hearn alisema macho yao sasa ni kukutanisha Muingereza Joshua na mshikilizi wa taji la uzani wa “heavy” la WBC, Deontay Wilder kutoka Marekani.

Wilder atatetea taji hilo lake dhidi ya Muingereza Tyson Fury mnamo Desemba 1, 2018. Kambi ya Joshua, ambaye anajivunia ushindi 22 (21 kupitia njia ya knockout), inataka pigano lijalo dhidi ya Mwamerika huyo lifanyike Aprili 3 mwaka 2018 jijini London. Wilder, 32, ameshinda mapigano 40 (39 kwa njia ya knockout).

Fury, 30, ameshinda mapigano 27 (19 kupitia njia ya knockout). Povetkin sasa ana rekodi ya ushindi 34 (24 kwa njia ya knockout) na amepoteza mapigano mawili.