Michezo

Bondia Nick 'Commander' Okoth ajikatia tiketi kushiriki Olimpiki 2020

February 27th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BONDIA Nick “Commander” Okoth amepata zawadi ya mapema ya siku yake ya kuzaliwa kwa kujikatia tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki 2020 katika uzani wa kilo 57 (Featherweight).

Hii ni baada ya Okoth, ambaye atasherehekea kufikisha umri wa miaka 37 Jumanne ijayo (Machi 3), kulemea Mganda Isaac Masembe kwa wingi wa alama katika mchujo wa Bara Afrika unaoendelea mjini Dakar nchini Senegal mnamo Jumatano usiku.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya masumbwi ya Kenya inayofahamika kama Hit Squad, anarejea katika Olimpiki baada ya miaka 12. Alishiriki Olimpiki 2008 mjini Beijing nchini Uchina alikoondolewa na Khedafi Djelkhir (Ufaransa) katika raundi ya 32.

Hakufuzu kushiriki Olimpiki 2012 mjini London nchini Uingereza na Olimpiki 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.

Okoth ndiye mwanamume pekee kutoka Kenya amefuzu kushiriki Olimpiki 2020 baada ya Rayton Okwiri (Middleweight), Hassan Shaffi Bakari (Flyweight), Elly Ajowi (Heavyweight), Joseph Shigali (Lightweight), Boniface Mugunde (Welterweight), Humphrey Ochieng’ (Light Heavyweight) na Fredrick Ramogi (Super Heavyweight) kubanduliwa nje.

Mabondia wanawake wa Kenya pia wameonyeshwa kivumbi mjini Dakar. Elizabeth Andiego (Middleweight), Evelyne Akinyi (Lightweight), Elizabeth Akinyi (Welterweight) na Beatrice Akoth (Featherweight) walizidiwa maarifa mapema.

Christine Ongare atakuwa na fursa ya mwisho kuingia Olimpiki atakapochapana na Mganda Catherine Nanziri katika mechi ya kuamua nambari tatu katika uzani wa kilo 51 (Flyweight) baadaye leo baada ya kupoteza dhidi ya Rabab Cheddar (Morocco) katika nusu-fainali Jumatano.