Bondia Okwiri apiga dafrau Fidel Munoz wa Colombia

Bondia Okwiri apiga dafrau Fidel Munoz wa Colombia

NA CHARLES ONGADI

BONDIA Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri alimnyuka Fidel Monterrosa Munoz wa Colombia katika raundi ya pili kwa njia ya KO nchini Marekani, Jumamosi.

Pigano hili la uzito wa Middle lisilo la kuwania taji lolote, lilikuwa la kwanza tangu Okwiri atue nchini Marekani kwa mapigano ya kulipwa chini ya udhamini wa kampuni ya Reyes Boxing Inc.

Ushindi huu umeboresha rekodi ya Okwiri tangu ajiunge na ndondi za malipo mwaka wa 2017 akishinda mapigano 8 na kutoka sare mara moja na kufikia sasa hajashindwa.

Kwa upande wake, Munoz ameshinda mapigano 39 na kushindwa mara 26 huku akiandikisha sare mara moja katika mapigano 66 aliyoshiriki tangu kujiunga na ndondi za malipo mwaka wa 2006.

Katika pigano hili, Okwiri alitumia raundi ya kwanza kumsoma mpinzani wake kwa ngumi za kushtukiza za tumbo, kichwa na kifua.

Baadaye aliamua kumaliza kazi mapema katika raundi ya pili kwa ngumi za kushoto na kulia zilizomwangusha Fidel chini kama gunia la chumvi.

Refa wa pigano hili alilazimika kuruka kati kusimamisha pigano hili ambalo limekuwa kichocheo cha Okwiri ambaye ni bingwa wa taji la Afrika la (ABU) kung’ara katika mashindano mengine yajayo.

Kabla ya pigano hili, Okwiri aliwahakikishia mashabiki wake ushindi kabla ya raundi 8 kutokana na alivyohisi kuwa katika ubora wa hali ya juu.

Mwamba huyu ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ‘ Hit Squad ‘ aliondoka nchini mwezi Mei mwaka huu kuelekea nchini Marekani kwa maandalizi yake baada ya mkata wa miaka mitano na kampuni ya Reyes Boxing Inc.

Okwiri aliyeanza mchezo wa ndondi mwaka wa 1999 mjini Mombasa kabla ya kusajiliwa na klabu ya Magereza, analenga kunyanyua taji la dunia katika kipindi cha miaka mitano atakayokuwa nchini Marekani.

Okwiri ambaye ni afisa wa Magereza mwenye cheo cha Sajenti, anawamiminia pongezi maafisa wa Magereza wakiongozwa na Generali Wycliffe Ogallo, naibu wake Benjamin Njoga na mwanariadha wa zamani kimataifa nchin Catherine Ndereba kwa ushirikiano wa dhati waliompatia.

You can share this post!

Kituyi apuuzilia mbali mkutano wa Raila na OKA

Ondoka Jack Grealish, ingia ?kiungo stadi Emi Buendia!