Michezo

Bondia Tyson Fury ataka mkewe amfyatulie watoto 10 wafunge kazi!

March 30th, 2024 2 min read

IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO

BONDIA matata raia wa Uingereza, Tyson Fury, amedokeza kuwa yeye na mkewe Paris Fury wanatarajia mtoto wa nane pamoja.

Mchapanaji huyo wa uzani wa Heavy Weight alishirikiana na Paris majuzi kutoa muhtasari wa maisha yao pamoja kupitia kipindi ‘At Home With The Furys’ kwenye Netflix.

Wawili hao ni wazazi wa watoto saba na wamekuwa katika ndoa kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita. Mtoto wao wa saba, ambaye ni wa kiume, alitua duniani miezi sita iliyopita.

Kwa mujibu wa Fury, 35, kizazi chake na Paris, 34, bado kinaongezeka na mpango wao ni kupanua familia hadi iwe ya watoto 10.

Majuzi, mwanamasumbwi huyo alitumia mitandao ya kijamii kutoa maoni kuhusu picha ya mkewe ambaye sasa ni mjamzito.

“Oneni mke wangu mjamzito alivyo mrembo. Yaani keshafyatua vimalaika saba tayari na bado ana nguvu tu! Tutahesabu watoto hadi wafikie 10. Mtoto nambari nane yu njiani na tunamtarajia duniani hivi karibuni!” akaandika kwenye Instagram.

Fury alikutana na Paris mara ya kwanza kipusa huyo akiwa na umri wa miaka 15, Hata hivyo, hawakuanza kuchumbiana hadi baada ya Paris kutinga miaka 16 kisha wakafunga pingu za maisha mjini Doncaster, Uingereza, mnamo 2008.

Fury pia alifichua kiini cha uamuzi wake wa kuwapa baadhi ya watoto wake jina ‘Prince’ kwa kusema: “Mimi ni mfalme na wao ni wakuu wangu ndipo wakapewa jina hilo.”

Bondia huyo alikutana na Paris mara ya kwanza kipusa huyo akiwa na umri wa miaka 15, Hata hivyo, hawakuanza kuchumbiana hadi baada ya Paris kufikisha umri wa miaka 16.

Walifunga pingu za maisha katika eneo la Doncaster nchini Uingereza mnamo 2008.

Kupitia kipindi cha ‘The Gypsy King’ wiki hii, Fury alisema: “Nimetafakari sana kuhusu uhusiano wangu na Paris. Tulianza kwa kuwa marafiki wa dhati kisha tukaoana. Alikuwa nami hospitalini kila nilipokuwa mgonjwa.”

“Nina deni lake kubwa sana ambalo nastahili kulipa. Niko radhi kutoa kila kitu changu kwa ajili ya Paris. Bila yeye na watoto hawa kuwa karibu nami, sidhani kama ningekuwa naona thamani ya maisha jinsi hali ilivyo hii leo.”

Akizungumza kuhusu mumewe kwenye kipindi chao cha ‘At Home With The Furys’, Paris alisema: “Ninampenda Fury kama mboni ya jicho langu. Ninamstahi sana kwa penzi la kweli na nitampenda daima. Anabadilika kila mwaka kuwa mtu mzuri zaidi.”