Michezo

BONGE LA SKENDO: Usajili wa Antoine Griezmann ni balaa tupu

July 26th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

UTATA unaozingira uhamisho wa mshambuliaji matata Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid hadi Barcelona unaonekana haukaribii kumazilika hivi karibuni baada ya ripoti kuwa Ligi Kuu ya Uhispania (LaLiga) inaweza kuufutilia mbali.

Mfaransa huyu alijiunga na mabingwa hao wa Uhispania wiki mbili zilizopita. Ameshachezea waajiri wake wapya mechi na ana jezi ya kuthibitisha amefanya hivyo.

Hata hivyo, ripoti nchini Uhispania zinasema kuwa uhamisho huo bado unaweza kubadilishwa kutokana na utata kuhusu ada ya uhamisho.

Ripoti hiyo ya kushangaza inatoka kwa shirika la BBC kupitia redio ya Onda Cero, ambayo inadai kuwa Atletico inalia kuwa ilichezewa shere kuhusu ada ya uhamisho ya Sh13.8 bilioni.

Na sasa, Rais wa La Liga, Javier Tebas, amekiri kuwa kuna sheria inayoweza kubadilisha uhamisho huo, licha ya kuwa Griezmann ameshavalia jezi ya Barca na kuichezea katika mechi za kujiandalia msimu mpya baada ya hafla ya kukata na shoka ya kutambulisha supastaa huyu Camp Nou.

“Inawezekana kuzuia uhamisho wa mchezaji,” Tebas aliambia Onda Cero.

“La Liga italazimika kuamua hatua itakayochukua. (Atletico) iliwasilisha malalamishi na kutufanya tuingiwe na shaka kupatia Barca leseni ya Griezmann.

“Kuna mpango maalumu unaoandaliwa. Wale wanaohusika katika kuuendesha watakuwa na majukumu ya kusuluhisha kesi hii.”

Hoja ambayo Atletico inawasilisha ni kuwa Barcelona ilisubiri hadi Julai 1 ipite ili ada ya uhamisho ya Griezmann iteremke kutoka Sh23.1 bilioni hadi Sh13.8 bilioni ndiposa iokoe mabilioni hayo. Barcelona kisha ililipa ada hiyo iliyopungua kulazimisha uhamisho wake Julai 12 na kuokoa karibu Sh14 bilioni.

Hata hivyo, Atletico inadai kuwa njama hiyo ilifanywa mapema kabla ya Julai 1 na kwa hivyo, Barca inafaa kulipa tofauti hiyo ya Sh9 bilioni.

Litakuwa tukio la kushangaza kuona Griezmann akilazimishwa kurejea Atletico kwa sababu ya sheria kuvunjwa.

Klabu ya Barca, ambayo ina hela nyingi, haitarajiwi kuruhusu hilo litendeke.

Huenda Barca ikalazimika kufanya mazungumzo na Atletico tena ili kufikia mapatano.

Griezmann alijiunga na Atletico mwaka 2014 akitokea Real Sociedad kwa Sh3.4 bilioni.

Alikuwa katika klabu ya chipukizi ya Sociedad kati ya mwaka 2005 na 2009 alipoingia timu ya watu wazima na kuichezea mechi 180 na kuifungia mabao 46.

Kabla ya kusaini kandarasi ya miaka mitano na timu ya watu wazima ya Sociedad, Griezmann alikuwa amevutia klabu za Lyon, Saint-Etienne na Auxerre nchini Ufaransa na Manchester United na Arsenal nchini Uingereza.

Alinunuliwa na Atletico mnamo Julai 2014.

Baada ya miezi mingi akihusishwa na uhamisho hadi Barca kwa Sh11.5 bilioni msimu 2017-2018, Griezmann aliongeza kandarasi yake na Atletico mnamo Juni 19 mwaka 2018 hadi mwaka 2023. Hata hivyo, ripoti zilisema kuwa siku chache baadaye, alianza kujutia uamuzi wa kusalia uwanjani Wanda Metropolitano. Alitangaza mwezi Mei mwaka huu kuwa ataondoka Atletico kujiunga na Barca. Alitua Barca mnamo Julai 12 kwa Sh13.8 bilioni, bei ambayo Atletico haijaridhika nayo.