Makala

BONGO LA BIASHARA: Anapata riziki kwa kupanda na kuuza miche mjini Kitale

March 5th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

UPANZI wa miti ni hatua muhimu katika juhudi za kuhifadhi mazingira.

Mbali na kudhibiti hali ya hewa, uhifadhi wa mazingira pia una nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii kiuchumi.

Katika mji wa Kitale, AkiliMali ilikutana na Bw Juma Wasike mwenye umri wa miaka 53. Yeye hufanya kazi ya kupanda na kutunza miche kabla ya baadaye kuiuza.

Ameifanya kazi hii kwa muda wa zaidi ya miaka 30 sasa na anasema kuwa miti ina faida nyingi kwa binadamu na kwa mazingira vilevile.

Isitoshe, anakiri kwamba kazi hii imemfaidi pakubwa kwa miaka hii yote kwa kumpa mapato ya kila siku. Alipoanza kazi hii akiwa kijana mdogo, kilichomchochea sana wakati huo ni shauku ya kutaka kuhifadhi mazingira. Hapo, akaanza kutayarisha miche nyumbani kwao kisha kutembea barabarani na katika makazi ya watu akiuza katika maeneo mbalimbali viungani mwa mji wa Kitale.

Bw Wasike kwa sasa ana sehemu ya ardhi anakofanyia kazi yake ya kupanda si tu miche ya miti pekee, bali pia matunda na maua. Hapa, ana miti ya aina mbalimbali ikiwemo ile ya kiasili na ya kigeni.

Ili kukabiliana na hali ya ukosefu wa maji nyakati nyinginezo, amechimba kisima ambacho humpa maji ya kunyunyizia miche hii.

Bw Wasike anapanda na kuuza miche ya matunda aina mbalimbali ambayo huwa anaiuza kati ya Sh200 na Sh400.

Miche ya maua huwa anauza kati ya Sh30 na Sh100. Vilevile, ana miche ya miti ya kila sampuli ambayo yeye huwauzia wateja kwa bei ya kati Sh20 na 300. Hata hivyo, kuna aina nyingine ya miti ambayo huwa anauza hata kwa Sh500 au Sh1,000.

Kwa mujibu wa Bw Wasike, huwa anatoa mchanga anaoutumia kwa makuzi ya miche msituni kwani una rotuba nyingi huku akitumia mbolea ya kiasili pia kutoka kwa kinyesi cha ng’ombe anaowafunga nyumbani kwake.

Kwa sasa, Bw Wasike ana jumla ya wafanyakazi 12 ambao yeye huwaajiri kwa misimu.

Yeye huwapa vibarua vya kupanda na kunyunyizia miche maji pamoja na kuendesha shughuli nyinginezo za kutunza miche hii.

Kila siku, huwa anaanza kazi yake saa mbili asubuhi na kuifunga saa kumi na moja jioni.

Wateja wake ni pamoja na wapiti-njia kwenye barabara za kuingia na kutoka mjini Kitale.

Aidha, ana watu wanaomfahamu vyema kiasi kwamba baadhi humpigia simu ili awapelekee miche kwani amejishughulisha na kazi hii kwa miaka mingi. Wanaonunua huwa inategemea kiasi wanachhitaji kwa sababu kuna wale ambao hununua miche mingi kwa pamoja hata zaidi ya miche 100 na kuna wale wananunua kwa kiasi kidogo tu.

Kazi hii imemfaidi kwa miaka mingi na kwake, huwa inampa riziki ya kila siku. Kufikia sasa, imemwezesha kuwaelimisha wanawe sita hadi kufikia kiwango cha vyuo vikuu. Isitoshe, ameweza kununua kipande kingine cha ardhi mjini Kitale ambako amejenga nyumba za kukodisha.

Kadhalika amepanua kiwango cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na chanzo cha haya yote ni kazi hii ambayo kwa mujibu wake, ni ya baraka kubwa.

Baadhi ya changamoto ambazo huwa anakumbana nazo ni kushuka kwa kiwango cha mauzo katika misimu ya kiangazi kwani wakati huu, wateja huwa hawanunui miche kwa wingi.

Pia maradhi ya miche huwa yanaathiri sana kazi hii haswa ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya miche ya spishi fulani za maua, matunda na miti ambayo huathiriwa sana na baridi kali, wadudu au hata kiangazi.

Kwa sasa, tamanio lake ni kuanzisha taasisi ambayo itakuwa ikiwaelimisha vijana kuhusu namna ya kukuza na kutunza miche pamoja na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kupitia upanzi wa miti.

Ombi lake kwa serikali kuu kupitia kwa Shirika la Misitu la Kenya ni ushirikiano ili waweze kupanda miti zaidi katika misitu ya serikali na shirika hili liwahusishe kwa kupata miche kutoka kwa wafanyabiashara sampuli yake.

Kwa mtazamo wake, serikali ya kaunti inapaswa ishughulikie maslahi yao kwa kuhakikisha kwamba maji ya mifereji inapatikana katika misimu yote. La mno katika wito wake, ni serikali ya kaunti iwanunulie aina mbalimbali za miche ya kupanda katika maeneo yote ya ardhi wanayomiliki ndani na nje ya Kaunti ya Trans-Nzoia.