Makala

BONGO LA BIASHARA: Mafunzo yalivyomsaidia kufaulu kilimo cha mboga

July 25th, 2019 3 min read

Na GRACE KARANJA

BW Eric Mwebi ni mzaliwa wa kijiji cha Kanyimbo, Kaunti ya Kisii.

Anasema kwamba kilimobiashara cha sukumawiki ni njia mojawapo ya kujiinua kimaisha lakini wengi hawana ujuzi kwa sababu wanawadharau wataalamu wa mmea huu.

Anaeleza njia rahisi za kupanda mboga hizi za sukumawiki kwa kutumia mfumo wa unyunyiziaji maji kwa njia ya matone maarufu kama drip irrigation.

Ujuzi wake ulitokana na mahangaiko ya muda mrefu ya kusaka vibarua ambavyo vimekuwa nadra sana kwa vijana.

Hata hivyo, kuna wanaodai kwamba vijana wanakikicha kilimo na kuwaachia wazee.

Mkulima huyu mwenye bidii alialika Akilimali katika shamba analolisimamia la Murumba lililoko eneo la Korompoi, Kaunti ya Kajiado.

Mtaalamu Eric aonyesha mimea ya nyanya ambayo imemaliza muda wa miezi miwili tangu kupandwa. Picha/ Grace Karanja

Safari yake ya kilimo ilianzia katika taasisi ya mafunzo ya kilimo ya Latia Resource Centre mwaka 2015, ambapo alipokea mafuzo ya mimea aina ya mboga tofauti kwa muda wa mwaka mmoja unusu.

Anasema taasisi za kilimo zinafaa kuongezwa humu nchini, kilimo ikiwa ni mojawapo ya ajenda kuu nne za serikali, ili iwe njia ya vijana kunusuriwa kutoka mikononi mwa uhalifu unaoendelea kuwapumbaza na kuharibu maisha ya vijana wengi nchini.

“Niliamua kujiunga na taasisi ya kilimo kwa sababu sikutaka kuendelea kuupoteza muda wangu nikitafuta kazi ambazo sikuzipata. Kwa sasa sijuti kamwe kwani ninaweza kujipatia mapato kutokana na kilimo cha mboga hii aina ya sukuma wiki ambayo wengi huona kama haina pesa,” alieleza mtaalamu huyu wa kilimo cha mboga Eric Mwembi.

Hata hivyo, anasema kwamba mara kwa mara yeye hupenda kulima mseto wa nyanya na sukuma wiki ili aweze kuligawa shamba lake vizuri katika vipande tofauti.

Pia kwa sababu huwezi kutabiri soko la humu nchini kwa sababu ya mazao yanayoingizwa humu nchini kutoka nchi jirani za afrika mashariki.

“Sababu kuu ya mimi kulima mazao ya sukuma wiki na nyanya ni kujaribu kukabiliana na bei za mazao yanayotoka nchi jirani kama vile Tanzania na Uganda, ambayo hufurika katika masoko tunayotegemea kuuza biddhaa zetu,” anaeleza.

Licha ya changamoto hizo na nyinginezo, mkulima huyu anasema ameshuhudia matunda yanayotokana na kilimo cha aina za mboga akisema ni pesa ambazo zinahitaji subira ambayo amejifunza kuwa nayo.

Sasa anakiri kwamba nia yake ni kuwa mtaalamu wa hali ya juu katika kilimo ili aweze kuwasaidia wakulima chipukizi ambao pesa zao nyingi hutumika vibaya wakijaribu njia za kufanikisha kilimo pasipo kufaulu.

Kwa juma la kwanza alipoanza kuvuna alitia mfukoni Sh8,000 katika kipande cha robo ekari huku akitarajia faida zaidi katika miezi mitatu ijayo hadi pale atakapong’oa mimea hiyo na kupanda mingine.

Changamoto

Anasema anapenda kilimo cha nyanya lakini kina changamoto nyingi ikilinganishwa na kilimo cha sukuma wiki ambacho ni rahisi.

Katika kupanda na kutunza mimea ya sukumawiki mkulima hachukui muda mwingi kama vile katika kilimo cha nyanya na mimea mingine, ikizingatiwa kuwa mmea huu hauna adui pamoja na magonjwa mengi ya kuwashambulia.

“Katika uzoefu wangu wa kulima mazao ya kuvunwa kwa muda wa miezi mitatu, nimegundua kwamba mmea wa sukuma wiki hauna changamoto nyingi kama vile nyanya ambazo pia mimi hulima. Muda wa kuangalia sukuma wiki pia ni mchache sio kama mmea wa nyanya ambao lazima uutunze kama mtoto mchanga,” anaeleza mtaalamu Mwebi.

Anasema kwamba gharama ya ununuzi wa mbegu za sukumawiki ni rahisi ukilinganisha na mbegu za mmea wa nyanya kwani ukiwa na Sh180 mkulima ana mbegu za kutosha kuanzisha kilimo hiki.

Anasema mbegu hizi zinapopandwa huchukua muda wa mwezi mmoja katika kitalu kabla ya kuhamishiwa shamba kuu.

Mbegu zingine za sukuma wiki huweza kuvunwa hadi miaka miwili hasa kwa wale walio na mashamba makubwa ambapo hawahitaji kuvuna kwa haraka ili kubadilisha mazao.

Anasema baada ya mimea ya sukuma wiki kukomaa majani yake yanaweza kuchumwa hadi miezi mitano lakini mitatu ya kwanza ndio ina faida zaidi.

Yeye hachagui wateja kwani hata wale ambao hununua mboga za matumizi ya moja kwa moja humfaidi sana kwa sababu ni wengi. Yeye huuza kilo moja ya sukuma wiki kwa Sh40.