Makala

BONGO LA BIASHARA: Mradi wa kukausha mboga wafaa wenyeji na wakimbizi

November 28th, 2019 2 min read

Na SAMMY LUTTA

UKOSEFU wa miundomsingi bora kama vile barabara inayounganisha Kaunti ya Turkana na sehemu nyingine nchini Kenya pamoja na kiangazi cha muda mrefu vimesababisha maelfu ya wakazi kutopata chakula bora kinachohusisha mboga na matunda.

Mboga na matunda ambayo inakuzwa kupitia ukulima wa unyunyuziaji maji mashamba kwa kiwango kidogo na zile ambazo hutoka Kaunti jirani za Pokot Magharibi na Trans Nzoia kupitia barabara ya Kitale- Kapenguria- Lodwar ni kama dhahabu sehemu hii, ikiwa bado ni safi.

Inalazimu wauzaji kupandisha bei kwa sababu wateja ni wengi sana. Changamoto hutokea wakati majambazi wanaposhambulia madereva wa kusafirisha mboga na matunda, mafuriko na magari kuharibika njiani na kusababisha bidhaa hizo zikifika sokoni kuuzwa kwa muda mfupi kabla ya kubaribika na kutupwa.

Josephine Abuba, 22, Mkimbizi kutoka makazi ya Kalobeyei kilomita chache kutoka kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi amekuwa miongoni mwa watu ambao kwa muda mrefu wamelazimika kukosa vyakula ambavyo havina vitamini.

“Ndio mboga ama matunda itufikie huku Kakuma, itachukua siku mbili kutoka Kitale na wakati wa mafuriko masoko hukosa kwa sababu eneo hili mtu hutafuta maji ya matumizi nyumbani. Wanaofaulu kusajiliwa na wafadhili kujiunga kwa miradi ya ukulima baada na kupata maji zaidi ya kunyunyuzia mimea maji ni wachache,” Abuba, Mkimbizi kutoka Sudan Kusini alieleza.

Hali hii ilimfanya kuwa miongoni mwa wakimbizi na wakazi eneo hilo walioteuliwa kujifunza ufumbuzi wa kudumu wa kutumia umeme-jua kwa kukausha mboga na matunda ili kuongeza thamani.

Kupitia Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lililopata ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya, alifunzwa jinsi atakavyotumia kifaa kinachotumia miale ya jua ‘sundrier’ kuhakikisha kila siku familia yake ina chakula bora.

Mbali na hiyo anatumia ufumbuzi huo kujitwika katika ujasiriamali.

Jumatatu tulipata Bi Abuya akielekea sokoni kununua mboga aina ya kunde. Kwa vile alifika sokoni saa moja asubuhi alifanikiwa kuwa miongoni mwa wanunuzi wa kwanza kupata mboga safi.

Aliyemwona sokoni ni kama alidhani Bi. Abuya alikuwa na wageni zaidi ya mia moja nyumbani ambao atapikia mboga hiyo.

Aliporudi nyumbani alidondoa, akaosha, akakatakata huku maji aliyoweka chumvi yakichemka.

Mboga zile zilitiwa kwa maji hayo na baada ya dakika mbili akatoa mboga hizo.

“Zikishatolewa kwa maji moto, unatumbukiza mboga ndani ya maji baridi mara mbili. Sasa unaweza kuanza kukausha. Chumvi tuliyoweka ni ya kusaidia mboga ibaki kuwa ya kijani kibichi,” akaeleza.

Bi Abuba anapeleka mboga hizo kwa Shule ya Msingi ya Morning Star ambapo anaweka kwa kifaa hicho cha kukausha na kungojea siku tatu ili atoe mboga hiyo ambayo itakuwa imekauka.

Bi Rhoda Daniel ambaye ni mwalimu katika shule hiyo anayesimamia ukulima na lishe bora, alihoji kuwa Bi Abuba, shule hiyo na wanawake kadhaa mjini Kakuma wanapata faida mara dufu kupitia uvumbuzi huo.

“Kwa sasa mboga ambazo zimekaushwa ni kama less ya akina katika benki kama hauna pesa unauza wakati wowote bila wasiwasi,” Daniel akasema.

Wanafunzi na familia ambazo zimekumbatia ufumbuzi huo wanapata chakula bora huku wengine wakitegemea nyama na ugali ana githeri pekee.

“Nimepewa jukumu la kufunza wanafunzi, wazazi na makundi ya wakulima jinsi ya kukausha mboga na kukula chakula bora. Kama shule tunauzia wakimbizi mboga zilizokaushwa na pesa tunazopata tunanunua sare za shule za wanafunzi wasiojiweza, kununua mbegu na kupanua shamba letu la mboga,” mwalimu huyo alieleza.

Mtu anapotaka kupika mboga hiyo, lazima kwanza aziloweshe kwa maji baridi ili ziwe rahisi kupika na pia kurudisha rangi yake ya mwanzoni na baadaye apike kama kawaida.

Wanaofadika katika mradi huo sasa wameanza kupanda mboga zao wenyewe ili wasitumie fedha mingi kwa kununua mboga.