Makala

BONGO LA BIASHARA: Sh100 za chama kila wiki zajengea wanabodaboda nyumba

April 18th, 2019 3 min read

Na PHYLIS MUSASIA

SH100 walizojikakamua kukusanya kila wiki kutoka kwa jasho la kuendesha bodaboda licha ya purukushani na askari wa serikali ya kaunti, ziliwezesha kundi la waendeshaji bodaboda kumi kutoka kaunti ya Nakuru limewawezesha kutabasamu ndani ya nyumba spesheli zenye vyumba viwili kila moja.

Wakiwa na uwekezaji ambao sasa umefika mamilioni ya pesa, kundi la Kianjahi Housing Cooperative Limited kutoka eneo la Barut Nakuru Magharibi, ni kielelezo kwa vijana nchini.

Maono ya kundi hili yalijitokeza mnamo 2015 lilipobuniwa kama chama cha kawaida naye Bw Benson Sigei akachaguliwa kuwa mwenyekiti.

Bw Peter Kariuki alichukua wadhifa wa naibu mwenyekiti huku Bw John Omondi akiwa mwekahazina.

Muda ulisonga na shughuli za chama zikawa zimeshika kasi na hapo ndipo wahusika waliamua kuongeza kiwango cha utoaji wa hela hizo kutoka Sh100 hadi Sh200 kisha Sh500 na baadaye Sh1000.

“Tulipohudhuria mkutano wa maendeleo kwa vijana Kitengela, tulipata mwanga mpya ndipo tukajadiliana jinsi ya kuanzisha chama kitakachotupa msingi bora wa maisha. Tulianza na Sh100 tu kwa sababu hicho ndicho kiwango ambacho kila mwanachama alisema angeweza kutoa kwa wakati huo,” akaeleza Bw Kariuki ambaye kwa sasa ni baba ya watoto wanne.

Alisema haikuwa rahisi kuongoza wanachama na kuwaahidi kuwa kungepatikana ufanisi kwani changamoto zilikuwa si haba.

Chama hicho baadaye kilifunguliwa na kufanywa huru kwa watu wengi ambao walitaka kujiunga nacho na idadi ya wanachama ikaongezeka hadi 70.

Bw Kariuki alisema kwamba sheria kali zilibuniwa kama vile wanachama kuhudhuria mikutano yote ya wiki bila kukosa na iwapo kulikuwa na wale waliokaidi sheria hiyo, walitozwa faini ya Sh500 mbali na mchango wa Sh1,000 uliokusanywa kila Ijumaa ya wiki.

Pesa zilizokusanywa zilikuwa nyingi na chama hicho kikawa sasa kinakaribia kufikia akiba ya milioni kadhaa kwenye akaunti kwenye benki ya Rafiki.

“Tulikutana wote baada ya mwaka mmoja mnamo Februari 2016 na tukaelewana kuwa kwa sababu akiba ilikuwa inakuwa kwa kasi, tulikubaliana kutafuta kipande cha ardhi. Wakati huo, tayari tulikuwa na maono ya kujengeana nyumba nzuri kila mmoja wetu japo baadhi ya wanachama walichukulia jambo hilo kama mzaha mara wengine wakikashifu maono hayo na kusema kuwa yalikuwa makubwa kuliko uwezo wetu,” akaeleza Bw Samuel Odhiambo ambaye ni mmoja wa wanachama wa Kianjahi.

Wanachama 40 baadaye walikihama chama hicho baada ya wale waliohusika kutafuta kipande cha ardhi kuangukia mikononi pa matapeli waliowahadaa na kutaka kuwaibia zaidi ya Sh600,000 pesa ambazo chama kilikubaliana zitumike kama amana.

Changamoto

Bw Odhiambo asema ulikuwa ni wakati mgumu kwa chama kwani waliotaka kuhama walitaka warudishiwe pesa zao zote na tayari chama kilikuwa mbioni kusimamisha shughuli nzima ya matapeli hao ambao walikuwa wameshaandikiwa hundi.

Wanachama walikuwa wameongezeka hadi 100 kabla ya pigo hilo kutokea lakini wale waliobaki waliendelea kujipa moyo huku wakiwa na maono ya kufaulu.

Bw Kariuki alieleza kuwa chama kilikuwa kimefunguliwa huru kwa kila aina ya watu wakiwemo walimu, madktari, mawakili na wafanyibiashara kutoka kila pembe ya nchi.

“Tuliona watu wengi wanaazimia kujiunga nasi na hivyo ikatubidi tuweke sheria kwamba kila aliyetaka kujiunga nasi alipe Sh15,100 kama ada ya usajili ili afikie umbali ambao wanachama wengine walikuwa wamefika,” akasema Bw Kariuki.

Ulipofika mwaka wa 2017, chama cha Kianjahi kilikuwa kimepanuka kwa kiasi cha haja na hapa mara moja ujenzi wa nyumba ukang’oa nanga. Wanachama walikuwa wamenunua sehemu ndogo ya ardhi katika eneo la Barut kwa ajili ya mradi huo.

“Tulianza na ujenzi wa nyumba 50 kwenye awamu ya kwanza ambapo kila nyumba mbili za familia tofauti zinachukua sehemu ya miguu 50 kwa 100 ya ardhi. Mradi huu ulikamilika kwa muda wa miezi mitatu tu kwa sababu hela hazikuwa shida,” akasema Bw Kariuki.

Bw Kariuki asema kuwa hatua hii iliwavutia watu wengi na idadi ya wanachama ikawa inaongezeka kila uchao. Kwani, ukiwa kulikojengwa nyumba hizi, unapata mtazamo mzuri wa ziwa lote la Nakuru.

Wanachama zaidi ya hamsini tayari wamewaonyesha visogo wamiliki wa nyumba za kukodisha mjini na kuhamia kwenye nyumba zao mpya. Ujenzi wa nyumba za awamu ya pili unaelendea na unatazamiwa kukamilika hivi karibuni.