Makala

BONGO LA BIASHARA: Vijana mafundi wa fanicha zinazopata wateja ng'ambo

September 12th, 2019 2 min read

Na RICHARD MAOSI

SIO lazima mtu kupata ajira ya ofisini ili aweze kukidhi mahitaji ya kila siku, hii ni kwa sababu vijana wengi siku hizi wanachukulia kazi za ufundi kuwa zinachosha au zisizopendeza.

Miongoni mwa vijana, utagundua ni asilimia ndogo sana yenye uwezo wa kurekebisha vyombo vilivyoharibika kama vile kurekebisha gurudumu la gari lililotoboka.

Kuunda bidhaa nzuri na thabiti nchi inaweza kuboresha ukuaji wa viwanda kwa kutengeneza vyombo vya kimsingi kama vile mabakuli, viti, meza, mapipa na masanduku kwa bei nafuu.

Haya ndiyo mawaidha kutoka kwa mratibu wa mafunzo ya ufundi katika taasisi ya Research Institute of Swahili Studies of East Afrika (RISSEA), Bw Maulid Kitito Omar inayopatikana mjini Mombasa.

Anasema mbali na vijana kupata maarifa ya vitabu ipo haja kubwa wapatiwe ujuzi wa kale unaoelekea kufifia, kama vile kutengeneza majahazi, ukulima na kukarabati vyombo vya samani.

Kitito alifichulia Akilimali kuwa RISSEA hailengi vijana waliosoma, ila inawapatia uwezo na ujuzi wa kujiajiri ili kukabiliana na janga la mihadarati na ukosefu wa ajira lililosheheni pwani.

Wakati tukizungumza na baadhi ya vijana wanaofanya useremala, walikuwa wakimalizia fanicha zilizokuwa zimeagizwa kwenda Uarabuni, labda kutokana na upekee wa mafundi kuendesha kazi kwa umahiri.

Fani yenyewe inahitaji mambo kadhaa kuzingatiwa kama vile mahitaji ya soko, na ushindani mkali unaopatikana sokoni ikizingatiwa kuwa ni watu wengi wanaojishughulisha na kazi ya kutengeneza samani.

Hata hivyo, Kitito anasema nguvu kazi na ujuzi wa kutosha ni baadhi ya mambo muhimu yanayohitajika katika shughuli nzima, ili kuhakikisha kuwa fundi anapata ufanisi mkubwa katika tajriba yake.

Kwa sasa RISSEA ni taasisi bora nchini kwa kutoa mafunzo ya kazi ya mikono na imechangia kwa asilimia kubwa ukuaji wa uchumi wa kaunti ya Mombasa kwa kuwatengenezea vijana nafasi nyingi za ajira.

Kitito alieleza kuwa mbali na kuwa na jukumu la kuandaa mafundi stadi, bado wanaamini kuwa wanachukua nafasi kubwa kwa kuenda sambamba na mahitaji ya kukuza viwanda vinavyohitaji ujuzi hasa katika sekta ya ufundi.

“Matamanio yetu ni kuhakikisha kuwa kila kijana anayejihusisha na taasisi hii anajipatia ujuzi wa kutosha kutosheleza mahitaji ya soko la kitaifa na kimataifa,” aliongezea.

“Mara nyingi tunalenga hoteli za kitalii na wasanii wanajifundisha fani ya kutengeneza samani. Kwa mfano Swahili door iliyotengenezwa kwa mti wa mvule (hardwood) inaenda hadi Sh180,000,” aliongezea.

Kuboresha karakana

Anasema suala la kuboresha karakana ya kutengenezea vyombo wamelipatia kipaumbele kwa sababu pana vyombo vya kutosha kutekeleza kazi za kila siku, hii ni kama vile randa za kulainisha mbao, wachongaji miundo, rangi na vifaa vinginevyo. Mbali na kupaka rangi, wana uwezo wa kuweka aina mbalimbali ya mapambo ya kiasilia kwenye samani, jambo linalowafanya wanunuzi wengi kutoka nchi za mbali kuwania bidhaa zao.

Bakari Mwakarimu ni mmoja wao ambaye anajipatia riziki kutokana na kazi za mikono hususan useremala. Anasema kuwa ingawa nafasi za ajira ni finyu siku hizi vijana wanaweza kuvumbua riziki kutokana na kazi kama hizi muradi ni halali.

“Vijana wanapaswa kujiwekea malengo na kufahamu kuwa maisha ni safari, wala wasikate tamaa kwa kile kidogo wanachokifanya kinaweza kuwafikisha mbali,” Bakari alitueleza.

Madirisha na milango wanayotengeneza ni nafuu na huchukua miundo mbalimbali ambayo huweza kumvutia mnunuzi kutokana na mapambo ya kila aina.

Ilipofika 2005 washikadau walipanua wigo na kuanzia hapo, ikawa lengo lake sio tu kazi za mikono bali pia utafiti katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya lugha, ukalimani na kujifunza lugha za kigeni.

Kitito alieleza kuwa RISSEA ilikuwa na tawi jingine katika kisiwa cha Lamu, ambapo vijana walipatiwa ujuzi wa kutengeneza majahazi kitengo kinachofifia.