Makala

BONGO LA BIASHARA: Kibanda kandokando ya Barabara Kuu champa tija

June 27th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUSTAWI kwa taifa kunategemea pakubwa uwezo wa wananchi wake kuwa wabunifu na kuvumbua mbinu mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi.

Kilimo ni tegemeo kubwa kwa makuzi ya taifa letu.

Namna ya kuuza mazao yanayotoka shambani ni jambo moja muhimu katika hatua za kuhakikisha kwamba mazao yamewafikia wanaoyahitaji.

Kwa sasa vijana wengi wanasema ya kuwa kupata kazi za ofisi ni vigumu na hivyo basi baadhi yao wanabuni namna za kujiajiri ili kupata mapato ya kujikimu maishani.

Katika eneo la V.I kaunti ndogo ya Mwea, Francis Machira ni mmoja wa vijana wanaojikimu kutokana na kujiajiri.

Machira, mwenye umri wa miaka 28, huwa anauza aina mbalimbali za matunda pamoja na mazao mengine kutoka shambani.

Alipokamilisha masomo yake ya shule ya upili mnamo 2009 katika eneo la Mwingi, Kitui, alikosomea, alianza kujishughulisha na vibarua vya hapa na pale na kuhifadhi hadi Sh36,000 alizozitumia kuanzisha biashara hii.

Mbali na nyanya, baadhi ya matunda ambayo huwa anauza ni pamoja na maembe, tikiti-maji, machungwa na parachichi.

Matunda haya huwa analetewa na wakulima kutoka mashambani ama wakati mwingine, yeye huyaendea mwenyewe kutegemea na mahitaji yake na ya wateja wake.

Mazao mengine kutoka shambani ambayo huwa anauza ni pamoja na viazi vyeupe, viazi vitamu, vitungu maji, pilipili mboga, dania, ndizi na maboga.

Mazao haya yote huwa anayauzia wapita-njia wanaosafiri kupitia Barabara Kuu ya Nairobi hadi Meru.

Kwa kawaida, wasafiri wengi wanaotumia magari ya kibinafsi na ya abiria vilevile hutua katika eneo hili kutokana na umaarufu wake wa wingi wa matunda ya kila sampuli ya kuuzwa.

Kununua bidhaa mashambani

Machira anaeleza ya kuwa kwa angalau siku moja kwa wiki, yeye huenda kununua baadhi ya bidhaa hizi mashambani kutoka kwa wakulima mbalimbali katika maeneo ya Kirinyaga na Nyeri. Kwa kawaida, bidha hizi huwa ananunua kwa wingi na kuzinunua kutoka kwa wakulima kwa vipimo vya kilo.

Hasa vitungu na karoti huwa ananunua kutoka eneo la Nyeri, matikitimaji kutoka eneo la Embu na Ukambani.

Ndizi na nyanya huwa anazinunua katika Kaunti ya Kirinyaga.

Hata hivyo, bei ya kununua na kuuza hulingana na msimu ulioko.

Wakati wa kiangazi kwa mfano, bei ya kununua na kuuza mara nyingi huongezeka maradufu. Na vilevile wakati ambapo hamna kiangazi, bei huwa ni ya chini mno.

Aidha, Machira anaelezea ya kuwa biashara hii ina manufaa kwake kwani anapata riziki ya kila siku yenye kumwezesha kulisha familia yake na kukimu mahitaji mengine ya kimsingi.

Kazi hii ndiyo kazi ya pekee ambayo anafanya na imemsaidia kufanya miradi mingine kama vile kununua ardhi na kujenga makazi mapya. Pia amefaulu kununua ng’ombe na mbuzi wachache.

Zaidi, kazi hii inampa mapato ya kuitunza familia yake ndogo ya mke na mtoto mmoja. Kwa sasa, anasema ya kuwa anapania kupanua biashara hii kwa manufaa zaidi.

Akifikia hili, pia atapata uwezo wa kuajiri vijana wengi zaidi kwani sasa ana wafanyakazi wawili wanaomsaidia katika kazi hii yake.

Baadhi ya changamoto ambazo anakumbana nazo ni ukosefu wa bidhaa haswa nyakati za kiangazi ambako pia bei huongezeka kwa kiwango cha juu mashambani.

Vilevile, wanunuzi hupungua wakati huu kwani bei ya bidhaa hizi huongezeka hadi sokoni.

Wakati mwingine bidhaa zinapokuwa nyingi sokoni, ushindani mkubwa huibuka na bei kushuka mno.

Anasema kuwa bidhaa nyinginezo hazikawii kwa muda mrefu, huharibika na kuwa hasara tele kwake.

Mwito wake kwa vijana ni wawe wabunifu na watafute namna mbalimbali za kujiajiri na wasitegemee kuajiriwa ofisini pekee. Pia wasichague kazi mradi tu wapate mapato ya haki na halali ya kuwawezesha kujikimu maishani.